1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafungwa wengine wawili wa Cuba waelekea Uhispania.

14 Julai 2010

Wizara ya mambo ya nje ya Uhispania yasema wafungwa wengine 3 watawasili leo kutoka Cuba.

https://p.dw.com/p/OIkY
Wafungwa wa kisiasa kutoka Cuba wawasili nchini Uhispania.Picha: AP

Ubalozi wa Uhispania nchini Cuba umesema kwamba Cuba imewaruhusu wafungwa wengine wawili wa kisiasa kuondoka kwenda Uhispania, siku moja baada ya wengine saba kuwasili nchini mjini Madrid. Kuondoka huko kumewaacha wafungwa wengine 11 wakiwa bado Cuba kati ya 20 ambao walikubali kuhamia Uhispania na ni kati ya idadi jumla ya wafungwa 52 ambao Cuba imekubali kuwaachia katika miezi michache ijayo.

Wafungwa wa kisiasa maarufu, Martha Beatriz na Oscar Espinosa wamesema waliwasiliana kwa njia ya simu na waandishi habari, Normando Hernandez mwenye umri wa miaka 40, Omar Rodriguez wa Umri wa miaka 44 na walisafiri kutoka Cuba wakiwa katika ya ndege ya shirika la Iberia jana jioni.

Wafungwa saba wa kisiasa wanaume walionyesha ishara ya ushindi walipowasili katika uwanja wa ndege wa Barajas ulioko katika mji mkuu wa Uhispania, Madrid katika ndege mbili wakiandamana na jamaa zao 33, baada ya ishara kubwa zaidi ya serikali ya kikomunisti ya Cuba katika kipindi cha mwongo mmoja.

Wafungwa hao saba ambao ni kati ya umri wa miaka 33 na 65 na ambao wote wana matatizo ya kiafya, walifungwa mwaka wa 2003 kutumikia vipindi vya kati ya miaka 15 na 24 gerezani. Tarehe 7 mwezi huu, Cuba ilikubali kuwaachia kwa utaratibu, wafungwa wa kisiasa katika mpango wa kushtukiza kati yake na kanisa Katoliki baada ya mgomo wa kususia chakula uliokaribia kifo cha mfungwa Guillermo Farinas.

Cuba inapania kuzuia marudio ya kifo gerezani cha mfungwa Orlando Zapata cha tarehe 23 mwezi Februari huku ikijaribu kuwa na uhusiano wa karibu wa kimataifa ili kuimarisha hali ya uchumi wake dhaifu.

Baada ya kupata habari juu ya makubaliano hayo kati ya kanisa Katoliki na nchi ya Cuba kuwaachia wafungwa wa kisiasa, mwanasaikolojia na mwandishi wa habari kwenye mtandao wa Internet na ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Cuba, Guillermo Farinas alisitisha mgomo wake wa miezi minne wa kususia chakula. Bw Farinas alisema mahojiano ya moja kwa moja ya rais wa zamani wa Cuba, Fidel Castro kwenye televisheni ya kitaifa, yaliashiria uungwaji mkono wa kimya kimya wa kuachiwa kwa wafungwa 52 wa kisiasa na kwamba hakuna chochote kilichobadilika katika kisiwa hicho cha kikomunisti.

Kulingana na tume ya haki za binaadam na maridhiano ya kitaifa ya Cuba, hata baada ya wafungwa hao 52 kuachiwa, bado kutakuwa wengine 115 walioko gerezani nchini Cuba. Hata Serikali ya Cuba imekana kwamba kuna wafungwa wa kisiasa ambao bado inawashikilia gerezani.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohamed