Wagombea 4,451 wapigania nafasi Bunge la Ujerumani
10 Septemba 2013"Wer die Wahl hat, hat die Qual" wanasema Wajerumani. Kwa Kiswahili tutasema "Hiyari isiyoradulika" - methali hiyo ina uzito zaidi katika uchaguzi mkuu wa tarehe 22 Septemba.
Mbali na vyama vikuu kama vile CDU,CSU,SPD au Walinzi wa Mazingira, kuna vyengine 29 vidogo vinavyopania kugombea viti.Tisaa kati ya vyama hivyo, vikiwemo chama cha Wasopiga Kura na kile kinachopinga sarafu ya euro, yaani chama cha "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani" vinavyogombea kwa mara ya kwanza kabisa viti vya Bunge la Shirikisho. Fomu za uchaguzi zitakuwa ndefu mfano wa kitambaa cha kupangusia sahani
Idadi kubwa ya vyama imesababisha kuwepo idadi kubwa pia ya wagombea. Jumla ya wagombea 4,451 wanapigania viti vya Bunge la Shirikisho - Bundestag. Hao ni wagombea 900 zaidi wakilinganishwa na idadi yao katika uchaguzi uliofanyika miaka minne iliyopita.
Msimamizi mkuu wa uchaguzi nchini Ujerumani, Roderich Egeler, anasema hili linatokana na mwamko wa umma.
"Tangu Ujerumani ilipoungana upya, idadi ya wagombea ilikuwa kubwa mara moja tu. Ilikuwa mwaka 1998. Ikilinganishwa na uchaguzi wa bunge mwaka 2009, safari hii idadi ya wagombea imeongezeka kwa watu 900. Hali hii, kwa maoni yangu, inazisuta zile hoja kwamba wananchi wamechoshwa na siasa." Anasema Egeler.
Bunge la viti 598
Miongoni mwa majukumu ya msimamizi mkuu wa uchaguzi ni pamoja na kuandaa uchaguzi na kuhakikisha sheria zinaheshimiwa. Egeler anadhamini na kusimamia data na maelezo yote kuhusu uchaguzi mkuu. Na yeye ndie atakayetangaza usiku wa tarehe 22 Septemba chama kipi kimejipatia kura ngapi.
Hadi wakati huu, kimoja tu ni dhahiri: bunge jipya la shirikisho - Bundestag, itakuwa na viti visivyopungua 598.
Ingawa kwa miaka minane sasa Ujerumani inaongozwa na mwanamke - Kansela Angela Merkel, lakini bungeni wanaume ndio wengi. Kwa mujibu wa data zilizotangazwa na msimamizi mkuu wa Uchaguzi, hali hiyo haitobadilika hata katika bunge jipya litakalochaguliwa Septemba 22 ijayo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo robo moja tu ya wagombea ni wanawake. Tangu uchaguzi mkuu wa amwaka 2009, idadi ya wagombea wa kike, haijaongezeka, badala yake imepungua.
Wanawake bado ni wachache
Idadi ya wagombea wa kike inatofautiana toka chama kimoja hadi chengine. Katika chama cha upinzani cha Walinzi wa Mazingira - Die Grüne - idadi ya wagombea wa kike inafikia asilimia 44. Idadi ndogo kabisa ni ya wagombea wa kike kutoka chama cha Kiliberali cha FDP, ambayo ni asilimia 20. Chama kinachopigania maslahi ya wanawake, wagombea wake wote ni wanawake.
Mwenye haki ya kuchaguliwa ni raia yeyote wa Ujerumani aliyefikia umri wa angalau miaka 18. Mgombea mmoja tu kijana hivyo anayegombea kiti cha Bunge la Shirikisho safari hii anatokea jimbo la kusini la Bavaria. Na mgombea mzee kuliko wote ana umri wa miaka 90, akiamini atakamilisha muhula wa miaka minne bungeni.
Egeler hakuweza kusema wagombea wangapi wana asili ya kigeni lakini la muhimu ni kwamba kila mgombea ana uraia wa Ujerumani, na la asili yake si muhimu hapo.
Mwaka huu wapiga kura milioni 62 wana haki ya kutoa sauti zao lakini katika uchaguzi wa mwaka 2009, karibu asilimia 30 ya watu wenye haki ya kupiga kura waliamua kusalia nyumbani na kuifanya idadi ya waliokwenda kupiga kura kuwa ndogo zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.
Mwandishi: Nina Werkhäuser
Tafsiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Josephat Charo