Viongozi wa Kiholanzi wakutana katika mdahalo wa kwanza
14 Machi 2017Nafasi ya Uholanzi katika Umoja wa Ulaya, ongezeko la wahamiaji nchini humo pamoja na mgogoro wa kidiplomasia na Uturuki ni miongoni mwa masuala yaliyotawala katika mdahalo huo.
Mdahalo huo unakuja wakati ambapo Uholanzi imezongwa na mzozo wa kidiplomasia na Uturuki. Siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu, Uholanzi imejikuta katika vita vya maneno na Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan, ambavyo vimempa Wilders uwanja wa kutangaza zaidi sera yake ya kupinga wahamiaji nchini humo.
Uturuki imesema itasitisha kwa muda mahusiano ya kidiplomasia na Uholanzi baada ya mawaziri wake kuzuiliwa kuwahutubia Waturuki wanaoishi Uholanzi katika mikutano ya kampeni. Aidha Uturuki pia imesema ndege yoyote itakayobeba wanadiplomasi wa Kiholanzi itapigwa marufuku kutumia anga la Uturuki.
Wakiwa katika mdahalo huo wa majibizano wa dakika 30 ambapo kila mmoja alipata nafasi ya kueleza mtazamo wake juu ya mustakbali wa Uholanzi katika siku za mbele, Wilders kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, kinachoupinga Umoja wa Ulaya na Uislamu cha Party for Freedom (PVV) alimwambia Rutte wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Freedom and Democracy (VVD) kuwa ameshikiliwa mateka na Erdogan na kumtaka afunge mipaka ya Uholanzi.
"Na bila shaka, nina hasira na Rais wa Uturuki Erdogan, lakini pia nina hasira na muhimili wa tano uliopo sasa Uholanzi, wa watu ambao hawataki kutangamana na jamii, ambao wanapuuza kanuni zetu na maadili yetu, ambao wanataka kututawala, na kututemea mate juu, na watu hawa wamepata nafasi kutokana na wanasiasa kama Mark Rutte," alisema Wilders.
Akimjibu juu ya suala la ongezeko la wahamiaji nchii Uholanzi, Rutte amemkosoa Wilders katika njia alizozitaja kuwa zingefaa kutumika kutatua tatizo hilo.
"Anataka kuondoa misahafu kila nyumba, mlango baada ya mlango, bado sijaelewa jinsi utakavyotekeleza hili, ningependa kujua polisi gani wa misahafu atakayetekeleza hili? Lakini kama hili ndiyo suluhisho lako, Bwana Wilders, kwa tatizo hili, suluhisho pekee ni kupunguza idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini na wale waliokuwepo tayari basi kuwaunganisha vizuri ndani ya jamii yetu na kuwa wawazi kabisa juu ya kanuni zetu na maadili yetu. Lakini sera yako inashauri kusafisha kwa fagio huku bomba bado likiwa linamwaga maji," amesema Rutte.
Na kuhusu suala la uwanachama wa Uholanzi ndani ya Umoja wa Ulaya, Wilders amesema katika mdahalo huo wa televisheni kuwa sasa ni wakati wa "Nexit" yaani Uholanzi kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya. Lakini Rutte alimpinga na kusema mapendekezo ya Wilders yataiweka Uholanzi katika hali ya hatari.
Matokeo ya uchaguzi wa Uholanzi yanatarajiwa kufuatiliwa kwa karibu na waangalizi wa Ufaransa, Ujerumani na Norway, nchi ambazo nazo zinajitayarisha kufanya uchaguzi baadae mwaka huu.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/dpa
Mhariri: Grace Patricia Kabogo