1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 150 wahofiwa kufa baada ya boti kuzama Libya

26 Julai 2019

Zaidi ya wahamiaji 150 hawajulikani walipo baada ya boti walizokuwa wakisafiria kuzama kwenye pwani ya Libya katika Bahari ya Mediterania.

https://p.dw.com/p/3MlmP
Migranten im Mittelmeer
Picha: picture alliance/AP Photo/O. Calvo

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR pamoja na walinzi wa pwani nchini Libya wamesema miongoni mwa wahamiaji hao ambao wanahofiwa wamekufa maji ni pamoja na wanawake na watoto.

Msemaji wa walinzi wa pwani ya Libya, Jenerali Ayoub Gassim amesema boti mbili zilizokuwa zimewabeba wahamiaji wapatao 300 zilizama umbali wa kilomita 120 mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Wahamiaji kadhaa waokolewa

Amesema kiasi ya wahamiaji 137 wameokolewa na wamerejeshwa Libya na hadi sasa walinzi wa pwani wamefanikiwa kuupata mwili mmoja.

Msemaji wa UNHCR, Charlie Yaxley amesema kuwa watu 147 wameokolewa hadi sasa na ameielezea ajali hiyo kama 'mbaya zaidi' kuwahi kutokea katika Bahari ya Mediterania kwa mwaka huu.

''Kundi la watu 300 liliondoka Khoms, Libya kwa boti. Tunaelewa kwamba walikuwa katika dhiki kubwa na awali waliokolewa na wavuvi wa eneo hilo na kisha na walinzi wa pwani ya Libya. Maafisa wetu walioko kwenye eneo la tukio wanawapatia msaada pamoja na huduma za matibabu,'' alifafanua Yaxley.

Libyen Luftangriff Tajoura Detention Center bei Tripolis
Wahamiaji kwenye kituo cha kuwashikilia wakimbizi Tripoli, LibyaPicha: Reuters/I. Zitouny

Yaxley amesema kwa mwaka huu mtu, mmoja alifariki akiwa njiani kutoka Libya kuelekea Ulaya kwa kila watu sita ambao walifanikiwa kufika katika mwambao wa Ulaya.

Janga baya kutokea mwaka huu

Mkuu wa shirika la UNHCR, Filippo Grandi amesema hili ni janga baya kuwahi kutokea kwa mwaka huu. Katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, Grandi amezitaka nchi za Ulaya kurejesha shughuli za uokozi katika Bahari ya Mediterania, ambazo zilisitishwa baada ya uamuzi wa Umoja wa Ulaya na ametoa wito wa kumalizwa kwa suala la kuwashikilia wakimbizi na wahamiaji nchini Libya pamoja na kuongeza njia salama nje ya Libya. Amesema hatua hizo zinapaswa kuchukuliwa sasa, kabla majanga zaidi hayajatokea.

Ajali ya kuzama boti hizo imetokea wiki chache baada ya wahamiaji wengine 68 kufa wakati boti iliyokuwa ikielekea Italia kuzama kwenye pwani ya Tunisia. Boti hiyo iliyokuwa na wahamiaji wengi wa Kiafrika, ilizama muda mfupi baada ya kuondoka kwenye mji wa Zuwara nchini Libya, kwa lengo la kufika Italia.

Mnamo mwezi Januari kiasi ya watu 117 walikufa au hawakujulikana walipo katika pwani ya Libya na wengine wapatao 65 walizama baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama kwenye pwani ya Tunisia mwezi Mei.