1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji waondoka Calais

26 Oktoba 2016

Serikali ya Ufaransa Jumatano hii imetangaza rasmi kuwa kambi ya wahamiaji iliyoko kaskazini mwa nchi hiyo ya Calais hivi sasa ni tupu, baada ya wahamiaji wote waliokuwa wakiishi kwenye kambi hiyo kuondoka.

https://p.dw.com/p/2RjrW
Frankreich Räumung Dschungel von Calais
Picha: Reuters/P. Rossignol

Maafisa wa eneo hilo wametangaza kuharibiwa kwa kambi hiyo iliotumiwa zaidi na wahamiaji waliokimbia vita na njaa na wamekuwa wakiishi kwenye mazingira duni kabisaa wakisubiri nafasi za kuingia nchini Uingereza kupitia njia ya chini ya maji maarufu English Channel.

Katika mpango wa kawaida, maafisa wa uhamiaji waliwasindikiza zaidi ya wahamiaji 5000 kwenye vituo vya kuombea hifadhi, ili kuanza upya kujiandikisha, huku zaidi ya wahamiaji 1000 wakiwa bado wapo kwenye vituo vya kusubiria kuondoka vilivyopo karibu na kambi hiyo.

Mmoja wa maafisa wa eneo hilo, Fabienne Buccio amesema hakuna mhamiaji aliyesalia kwenye kambi na kwamba wanaendelea na mpango huo kwa kuwaondoa kwa utaratibu maalumu.

Wahamiaji hao awali walionekana kutembea hovyohovyo kwa makundi makundi, hata baada ya kutangaziwa kuondoka kwenye eneo hilo. Hata hivyo mamlaka zimesema zitakamilisha mpango huo ifikapo jioni ya jumatano hii.

Wahamiaji hao wamekuwa wakiishi katika eneo la Calais kwa miongo kadhaa, lakini kukua kwa kambi yenyewe kumesababishwa na kuongezeka kwa tatizo la wahamiaji Barani Ulaya. Na wakati ilipoendelea kuwa na wahamiaji wengi wanaoungwa mkono na makundi ya misaada, hatimaye Ufaransa ikaamua kuifunga kambi hiyo.

Calais Räumung
Wahamiaji wakiondoka katika kambi ya Calais, ambayo waliichoma moto kabla ya kuondokaPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Camus

Kichochoro pekee kinachopitika kuelekea kwenye kambi hiyo iliyoko karibu na mji wa Calais kilichomwa moto usiku wa jumatano hii ikiwa ni siku ya pili ya kuwaondoa wahamiaji na kikosi cha zimamoto kilijaribu kuzima moto huo ili kuhakikisha hauleti madhara makubwa. Zaidi ya wahamiaji 100 waliondolewa kwenye eneo hilo.

Na huko Jijini London, Uingereza mwanamitindo Lilly Cole ameongoza maandamano yanayokusanyisha waandamanaji katika daraja la Millenium jijini humo, wakitaka Uingezrea kuwasaidia watoto waliokwama, baada ya serikali ya Ufaranmsa kuamua kuifunga kambi ya Calais. Cole, amekuwa miongoni mwa waandamanaji 100 waliobeba mabango na maumbo ya moyo yenye rangi nyekundu, wakitaka kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kuwapa makazi watoto wanaotoka kambi ya Calais.

"Tupo hapa tukisimama kwa umoja tukiwaunga mkono watoto wasio na usaidizi wa Calais, ili kuwaonyesha kwamba tunaelewa kuwa namna wanavyofanyiwa si sawa na haikubaliki, hivyo tunataka serikali ya Uingereza na Ufaransa kuharakisha kuwatafutia makazi", amesema mratibu wa maandamano hayo, Remi Olajoyegbe. 

Kulingana na taarifa za mamlaka, kambi hiyo iliyokuwa karibu na bandari ya Calais, ambayo pia imekuwa kitovu cha wahamiaji kutumia kutorokea nchini Uingereza, kwa kudandia magari makubwa ama treni zinazopita eneo hilo ilikuwa na wahamiaji 6300, ingawa makundi ya misaada yanasema idadi hiyo ilikuwa kubwa zaidi.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/EAP/DPAE.
Mhariri: Iddi SSessanga.