Wahaniaji wa Syria waingia Ujerumani kisheria
4 Aprili 2016Familia sita zenye kujumuisha wanaume, wanawake na watoto 32 zimewasili zikiwa kwenye ndege mbili kutokea Istanbul baada ya kuchaguliwa na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kama ni kundi la wanyonge ambalo ni rahisi kuathirika.
Kundi la kwanza la wakimbizi 16 lilichukuliwa na basi kupelekwa katika kituo cha mapokezi huko Friedland karibu na Gottingen kaskazini mwa Ujerumani kabla ya mchana. Kutoka hapo watasambazwa katika miji na jamii kadhaa katika jimbo la Lower Saxony. Kundi la pili la wahamiaji wengine 16 lilikuwa lifuatie baadae.
Waomba hifadhi hao walipokewa na wafanyakazi wa Shirika la Msaada wa Kiufundi la serikali ya Ujerumani (THW) na wale wa mamlaka ya uhamiaji (BAMF). Corinna Wicher wa mamlaka ya wahamiaji amesema baada ya kuwasili kwa kundi la kwanza la wakimbizi 16 kwamba walikuwa na hamasa kubwa na familia hizo zilikuja tu kujuwa wiki moja iliopita kwamba watasafirishwa kutoka Uturuki kuletwa Ujerumani.
Waliokataliwa hifadhi
Kwa mujibu wa makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki wahamiaji waliowasili Ugiriki baada ya tarehe 20 Machi ambao wameshindwa kuomba hifadhi au kushindwa kustahiki kupatiwa hifadhi watarudishwa Uturuki isipokuwa wale watakaoweza kuthibitisha kwamba wanakabiliwa na ukandamizaji nchini Uturuki.
Kivuko chenye watafuta hifadhi waliokataliwa kutoka kisiwa cha Chios nchini Ugiriki tayari kimewasili leo hii katika mji wa magharibi wa Uturuki wa Dikili ambapo kutoka hapo gavana wa mji huo Mustafa Topraka anasema watapelekwa katika kituo cha kupokea watu wa kurudishwa makwao.
(O-Ton Toprak)
"Watu hawa 202 watapelekwa katika kituo cha kuwarudisha makwao cha Kirklareli kwa kutumia basi baada ya kuteremka kwenye kivuko alama zao za vidole zimechuliwa na wamefanyiwa uchunguzi wa afya. Inaelezwa kwamba takriban wahamiaji wasio halali elfu tano wamewasili katika kisiwa hicho cha Ugiriki baada ya tarehe 20 Machi.Hatujuwi wangapi kati yao ni Wasyria na wangapi sio Wasyria na wangapi kati yao Ugiriki itawaleta Uturuki kwa kuzingatia makubaliano na Umoja wa Ulaya"
UNHCR kufuatilia makubaliano
Kwa kila mhamiaji anayerudishwa Uturuki mkimbizi mmoja wa Syria atachukuliwa moja kwa moja kutoka Uturuki na kupatiwa makaazi mapya Ulaya.
Msemaji wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa Melissa Fleming amesema wafanyakzi wa shirika hilo hapo awali wamezungumza na wale waliorudishwa Uturuki na hawakuelezea nia ya kutaka kupatiwa hifadhi.
Amesema makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki yanatarajiwa kuwachuja watu wanaohofia maisha yao au wenye ushahidi madhubuti wa kukandamizwa iwapo watarudishwa makwao au katika nchi nyengine.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa
Mhariri :Yusuf Saumu