1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri juu ya kudhibiti biashara ya silaha na kashfa ya Jerome Cahuzac

Abdu Said Mtullya4 Aprili 2013

Wahariri wanazungumzia mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kudhibiti biashara ya silaha duniani na juu ya mgogoro unaoikabili serikali ya Rais Hollande kufuatia kujiuzulu kwa waziri wake wa bajeti

https://p.dw.com/p/189Qg
Aliekuwa Waziri wa Bajeti nchini Ufaransa Jerome Cahuzac
Akiekuwa Waziri wa Bajeti,nchini Ufaransa ,Jerome CahuzacPicha: Getty Images/AFP

Gazeti  la "Straubinger Tagblatt" linasema mkataba uliopitishwa na Umoja wa Mataifa wa kudhibiti biashara ya silaha duniani ni kama sanamu tu.Mhariri wa gazeti hilo anautilia mashaka makubwa mkataba huo. Anatilia maanani kwamba zipo baadhi ya nchi zinazoupinga mkataba huo.

Naye Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Rundschau" anakumbusha kwamba biashara ya silaha inafikia dola Bilioni 70 kwa mwaka duniani.Na kwa hivyo suala la uchumi  lazima litiliwe maanani.Mhariri huyo anasema ilivyo kuhusu mikataba ya kimataifa, mkataba huo wa kudhibiti silaha pia una mapungufu mengi.

Mkataba utaleta manufaa:

Ukweli ni kwamba biashara ya silaha itatatizika hapa na pale.Lakini ikiwa nchi fulani inataka kuuza silaha bila shaka itatafuta njia ya kufanya hivyo.Inapasa kutilia maanani kwamba biashara ya silaha siyo suala la kisiasa tu bali pia ni la   kiuchumi. Lakini mhariri wa "Süddeutsche" anasema mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha utaleta manufaa.Kutokana na mkataba huo itakuwa vigumu kwa serikali haramu kupatiwa silaha,aidha itakuwa vigumu silaha kupelekwa katika sehemu za migogoro. Shinikizo la kuufanikisha mkataba huo litatoka kwenye mashirika ya kutetea haki za binadamu na asasi za kiraia.Jumuiya hizo zilionyesha ukakamavu katika maungumzo ya kuufikia mkataba huo.

Serikali ya Hollande matatani:

Serikali ya Ufaransa inakabiliwa na mgogoro kufuatia kujizulu kwa Waziri wa bajeti, Jerome Cahuzac kutokana na kashfa ya kukwepa kulipa kodi.Waziri huyo alificha  fedha zake kwa muda wa miaka 20 katika benki ya nchi za nje.

Juu ya kashfa hiyo gazeti la "Frankfurter Allgemeine"linasema tokea kuingia madarakani, serikali ya kisoshalisti ya Hollande ilikuwa inajaribu kutoa sura ya uadilifu. Lakini mwongozo wa uadilifu utakuwa na nguvu gani ikiwa hakuna imani?

Na mhariri wa "Saarbrücker" anaongezea kwa kueleza, kati ya watu wote, ni Waziri aliekuwa akitetea haki katika masuala ya kodi na sera ya kubana matumizi. "Kumbe yeye amezificha fedha zake katika benki za nje."

Mhariri anauliza,sasa ni nani tena wa kuaminika nchini Ufaransa? Anasema ukosefu wa uadilifu umesababisha mgogoro nchini Ufaransa na umewakumba viongozi wote wa kisiasa. Na mhariri wa "Berliner Zeitung" anasema kilichobakia sasa ni kutumai kwamba utakuwapo ujasiri wa kuanza mambo upya.

.Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Josephat Charo