Wahariri wa Ujerumani nao wamtaka Assad aondoke
28 Desemba 2011Juu ya mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Boko Haram, mhariri wa gazeti la Hessische/Niedersächsiche anasema ni wazi kwamba mashambulizi hayo yamewakasirisha watu nchini Ujerumani. Lakini anasema jambo muhimu ni kuweza kukitambua kiini cha mvutano wa kijamii nchini Nigeria.
Mhariri huyo anasema siyo kila mgogoro, unakuwa wa kidini, ati kwa sababu tu, unaonekana kijuujuu kuwa ni wa kidini. Mambo yanayosababisha mvutano nchini Nigeria ni pamoja na ufisadi, umasikini na dhulma.
Mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemiene anaiunga mkono hoja hiyo kwa kueleza kuwa hakuna dini inayotumiwa vibaya na watu wenye siasa kali kama ya Kiislamu mnamo karne hii.
Lakini anaeleza kwamba inafahamika kuwa kila mgogoro unazo sababu zake, kwa mfano, umasikini na udhalimu wa kisiasa. Lakini sababu hizo, linaeleza gazeti la Hessiche/Niedersächsiche, haziwezi kuihalalisha sera ya kuiandamana jamii fulani ya wachache nchini iwe ya Wakristo, Waislamu au ya Wayahudi.
Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linayazungumzia matukio ya nchini Syria baada ya kuwasili kwa wajumbe wa Umoja wa Nchi za Kiarabu nchini humo. Mhariri wa gazeti hilo anasema mpango wa kuleta amani uliopendekezwa na Jumuiya hiyo haulingani na hali halisi.
Mhariri huyo anafafanua kwa kusema kuwa mpango huo unavutia kwa nje, lakini hauwafiki na mazingira halisi yanayoikabili Syria. Wananchi wenye ghadhabu kubwa hawatalainishwa na mpango huo juu ya kuanzisha mazungumzo baina ya serikali na wapinzani. Wapinzani wa Syria hawatasimamisha harakati za upinzani mpaka hapo Rais Assad atakapoondoka madarakani.
Gazeti la Stuttgarter Nachrichten pia linatilia maanani kwamba ujumbe wa Umoja wa Nchi za Kiarabu upo nchini Syria. Lakini mhariri wa gazeti hilo anahoji kwamba mafanikio katika kuutatua mgogoro wa Syria hayatatokana na juhudi za ujumbe huo. Mhariri huyo anaeleza kuwa kuwasili kwa ujumbe wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu nchini Syria kumeanzisha hatua mpya katika harakati za upinzani.
Anasema mafanikio ya kuutatua mgogoro wa Syria hayatatokana na juhudi za ujumbe huo bali yatategemea na jinsi wapinzani watakavyoendelea kuubana utawala wa Rais Assad.
Mwandishi: Abdu Mtullya
Mhariri: Othman Miraji