Wahariri wamtaka Merkel aseme wazi, katika Jamhuri ya Czech
4 Aprili 2012Gazeti la"Volksstimme" linasema katika ziara yake katika Jamhuri ya Czech Kansela wa Ujerumani Angela Merkel angeliweza kusema wazi kwamba sera ya Jamhuri ya Czech ya kuupaka matope Umoja wa Ulaya haitavumiliwa tena. Lakini badala ya kuchukua hatua hiyo Kansela Merkel aliweka mkazo juu ya diplomasia na kuendeleza ushirikiano. Mhariri wa gazeti la "Volkssitimme" amesema katika ziara yake Bibi Merkel aliwasilisha hisia kana kwamba hakujali yanayowasumbua watu katika nchi hiyo.
Gazeti la "Reutlinger General Anzeiger" pia linalalamika juu ya ziara ya Kansela wa Ujerumani katika Jamhuri ya Czeck . Mhariri wa gazeti hilo anasema Bibi Merkel alipaswa kutoa kauli za uwazi katika ziara hiyo. Mhariri huyo anaeleza kuwa Kansela Merkel amejaribu kumwimarisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Czech Petr Necas ambae kwa upande wake amemhakikishia Kansela Merkel kuwa nchi yake itaitekeleza sera ya kubana matumizi na itafuata nidhamu ya bajeti bila ya kutia saini mkataba husika.
Gazeti la "Freie Presse" pia limeandika juu ya ziara ya Kansela Merkel katika Jamhuri ya Czech lakini kwa kulizingatia suala la nishati ya nyuklia.Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba Jamhuri ya Czech inakusudia kuongeza matumizi ya nishati ya nyuklia. Mhariri huyo anasema kile kinachofahamika ni kwamba hadi kufikia mwaka wa 2050 ,Jamhuri ya Czech inakusudia kuzalisha asilimia 80 ya nishati ya umeme kwa kutumia nguvu za nyuklia. Hizo ni habari zinazowatia wasiwasi walinzi wa mazingira nchini Ujerumani na Austria. Gazeti la "Freie Presse" linasema inapasa kutambua kwamba endapo yanatokea maafa ya kinyuklia, madhara yake hayatabakia ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Czech tu.Kwa hivyo ikiwa Kansela Merkel anayo dhamira ya kweli juu ya kuondokana na matumizi ya nishati ya nyuklia nchini Ujerumani basi itakuwa vizuri ikiwa ataiwakilisha kwa nguvu thabiti, sera ya nishati ya Umoja wa Ulaya katika ziara yake.
Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linatoa maoni juu ya mgogoro wa Syria. Mhariri wa gazeti hilo anauliza jee ni nani atakaefuatilia hatua ya kusimamisha mapigano nchini humo ikiwa itafikiwa? Mhariri huyo anasema hatua hiyo haitakuwa na maana yoyote ikiwa Rais Assad ataendelea kuwamo madarakani.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/
Mhariri:Mohammed Khelef