Wahouthi washambulia meli katika bahari ya shamu
6 Februari 2024Serikali nchini Yemen imesema meli moja iliyokuwa ikielekea kusini mwa bahari ya shamu ilishambuliwa na ndege isiyokuwa na rubani inayoaminika kuwa ya waasi wa Houthi, hili likiwa shambulizi lao la hivi karibuni katika kampeni yao ya kushambulia meli kufuatia vita vinavyoendelea kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza.
Waasi hao wamekuwa wakishambulia meli kadhaa kwa kutumia droni na makombora katika bahari hiyo kuanzia katikati ya mwezi Novemba kwa kile walichokielezea kwamba ni kusimama pamoja na watu wa Palestina dhidi ya vita vya Israel mjini Gaza.
Iran yasema haitosita kujibu mashambulio yatakayoilenga nchi hiyo
Msemaji wa jeshi wa kundi hilo amesema wamerusha makombora katika meli mbili ya Morning Tide na Star Nasia, zilizokuwa na bendera ya visiwa vya Barbados na Marshall zinazomilikiwa na Uingereza na Marekani.
Shirika la Ambrey la usalama wa majini limesema meli iliyokuwa na bendera ya Barbados inayomilikiwa na Uingereza iliharibiwa kufuatia shambulizi hilo la angani wakati ilipokuwa ikielea kusini mashariki mwa bahari ya shamu. Ambrey imesema hakuna hata mtu mmoja aliyejeruhiwa, ikiongeza kuwa meli hiyo baadae ilibadilisha njia na kuendelea na safari zake.
Naye Mmiliki wa Meli ya Morning Tide ya kampuni ya uingereza pia ya Furadino alisema kwa sasa meli yake inaelea bila matitizo yoyte bila kutoa maelezo zaidi. Hata hivyo Kiongozi wa wahouthi Abdul Malik al- Houthi, amesema kundi lake litaendelea kushambulia iwapo Israel haitositisha vita vyake mjini Gaza
Marekani yashutumiwa kuchochea vurugu zaidi Mashariki ya kati
Huku hayo yakiarifiwa Urusi na China zimeishutumu Marekani wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuchochea mgogoro wa Mashariki ya Kati kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Syria na Iraq.
Wahouthi wafyatua makombora kuelekea meli za kivita za Marekani
Siku ya Ijumaa jeshi la Marekani lilishambulia maeneo kadhaa katika nchi hizo mbili kama sehemu ya majibu ya mashambulizi ya droni yaliyofanyika Januari 28 katika kambi ya kijeshi ya Marekani iliyosababisha mauaji ya wanajeshi wake watatu.
Uingereza na nchi washirika washambulia maeneo ya Kihouthi Yemen
Hatua hiyo imeongeza wasiwasi kuwa vita vinavyoendelea kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas vinaweza kutanuka na kuathiri kanda nzima. Balozi wa China katika Umoja wa Mataufa Jun Zhang amesema matendo ya Marekani bila shaka yatasababisha msururu wa kulipiziana kisasi katika kanda hiyo.
Chanzo: ap/reuters