Wahouthi washambulia tena meli kwenye Bahari ya Shamu
5 Machi 2024Ripoti za awali zinaoesha kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya jana, ambapo meli hiyo iliyobeba makontena, MV MSC SKY II, ilishambuliwa kwa makombora ya Wahouthi.
Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi alisema siku ya Jumatatu (Machi 4) kwamba waliishambulia meli hiyo kwa makombora kadhaa.
Jeshi la Marekani lilisema Wahouthi walirusha pia makombora ya masafa ya mbali kuelekea kusini mwa Bahari ya Shamu, lakini hayakusababisha madhara yoyote kwa meli za Marekani.
Hata hivyo, Kamandi ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilifanya kile ilichokiita "mashambulizi ya kujilinda" dhidi meli makombora mawili ya kushambulia meli yaliyokuwa yanatishia usalama wa meli za biashara na meli za jeshi la Marekani kwenye eneo hilo.
Soma zaidi: Waasi wa Kihuthi waendelea na mashambulizi Bahari ya Shamu
Marekani na Uingereza zimeshafanya mashambulizi kadhaa dhidi ya Wahouthi ndani ya Yemen na ziliowatangaza tena kuwa magaidi.
Kutiribuliwa safari za baharini za kimataifa
Mashambulizi ya kundi hilo kwenye Bahari ya Sham yameharibu utaratibu wa usafirishaji mizigo kupitia bahari hiyo kwa kuzilazimisha meli kubadilisha njia na kutumia njia refu zaidi na zenye gharama kubwa zaidi kuzunguka kusini mwa Afrika.
Kwa upande mwengine, mashambulizi hayo yameongeza wasiwasi wa uwezekano wa vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kugeuka kuwa mgogoro wa kikanda na hata wa kimataifa.
Soma zaidi: Marekani yatishia mashambulizi zaidi Mashariki ya Kati
Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mawasiliano wa serikali ya Wahouthi, Misfer Al-Numair, alisema meli zote zinazopita kwenye eneo lao lazima kwanza zipate kibali cha Mamlaka ya Baharini ya Yemen.
Akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha Al Misrah, waziri huyo alisema kwamba wako tayari kusaidia maombi ya vibali na kuzitambulisha meli hizo kwa jeshi la Yemen kwa usalama wa meli hizo.
Soma zaidi: Mashambulizi Bahari ya Shamu yatikisa biashara duniani
Yemen ina mamlaka ya udhibiti wa meli 12 za bahari ya kimataifa inayoingia hadi kwenye ujia mwembamba wa Bab al-Mandab, ambao takribani asilimia 15 ya meli za kimataifa hupita wakati zikielekea au kutoka kwenye Mfereji wa Suez nchini Misri.
Katika nyakati za kawaida, zaidi ya robo ya meli za makontena duniani, zikiwemo zilizobeba vifaa vya ujenzi, magari, kemikali na mazao ya kilimo kama vile kahawa zinapitia Mfereji wa Suez.
Vyanzo: dpa, Reuters