Wahudumu wa afya Nakuru walalamikia mazingira duni ya kazi
20 Oktoba 2020Miezi saba baada ya kisa cha kwanza cha ugonjwa wa COVID 19 kuripotiwa nchini, waziri wa afya Mutahi Kagwe anaonya kuhusu uwezekano wa kutokea mlipuko wa pili wa maambukizi ya virusi vya corona nchini.
"Tunawaona hata wahudumu wa afya wakirejelea shughuli zao kama kawaida. Nyakati hizi si za kawaida, na tafadhali mzingatie kwamba msipochukua tahadhari, matokeo yatakuwa mabaya,” alisema waziri Kagwe.
Lakini wahudumu wa afya ambao wameyaweka maisha yao hatarini katika mapambano na ugonjwa huu, wanaonekana kukata tamaa kutokana na kile wanachosema ni mazingira duni katika maeneo ya kazi. Baadhi wametishia kugoma.
Soma zaidi: Jumla ya wauguzi 16 Kenya wapoteza maisha kutokana na COVID-19
"Hatuna vifaa vya kutosha vya kujikinga, wagonjwa waCOVID 19 wamechanganywa katika vyumba vya wagonjwa kwenye hospitali zetu pamoja na wagonjwa wa kisukari, maradhi ya ukimwi, kina mama waja wazito walioambukizwa, kati ya wengine," alisema Caroline Adwera, mmoja wa viongozi wa muungano wa wauguzi nchini, akizungumzia hali ilivyo kwenye hospitali kuu mjini Nakuru.
"Pia tuna wahudumu wetu wa afya walio na magonjwa haya na wanalazimishwa kuendelea kufanya kazi na kutangamana na wagonjwa hawa.”
Waziri wa afya wa kaunti ya Nakuru Kariuki Gichuki anashikilia kwamba, wahudumu wa afya pia ni wana jamii na si kweli kwamba wanaweza kuambukizwa ugonjwa huu wakiwa kazini pekee.
Gavana wa kaunti ya Nakuru Lee Kinyanjui amekiri kwamba kuna ongezeko la idadi ya wagonjwa, ingawa anashauri kwamba ni jukumu la kila mkenya kuhakikisha hali nzuri ya afya.
Soma pia: Majaribio ya chanjo ya COVID-19 yaidhinishwa Kenya
Kenya imerekodi vifo 17 vya wahudumu wa afya huku wengine 1231 wakiripotiwa kuambukizwa virusi vya corona.