1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahudumu wa malori wamulikwa juu ya utumikishwaji wa watoto

Wakio Mbogho10 Juni 2021

Hali ya wasichana wenye umri mdogo kutumiwa vibaya na wahudumu wa malori ya masafa marefu, ni jambo linalozidi kuibua wasiwasi, kwani ndoto za wengi wao hutibuka wanapapata ujauzito, magonjwa au kulazimika kuacha shule.

https://p.dw.com/p/3ugsm
Afrika Grenzübergang Stau LKW Kenia Uganda
Picha: Brian Ongoro/picture alliance

Serikali ya Kenya kwa ushirikiano na wadau wengine wamezindua miradi inayonuwia kubadili hali hii, ikiwa ni mojawapo ya juhudi za kufikia malengo ya maendeleo endelevu. 

Wakaazi wa eneo la Salgaa, kaunti ya Nakuru hawakuweza kuficha furaha yao kutokana na miradi ya maji na elimu iliyozinduliwa eneo hilo, ambalo ni eneo kame. 

“Kina mama wamefurahi. Jamii yote imefurahi. Hata watoto wetu kule shule wamepata maji masafi. Kutoka sasa chakula na mboga, hakitaenda kuchukuliwa Molo kuja hapa Salgaa kwa sababu wataliam nyumbani. Ng’ombe wataweza kutoa maziwa ya kutosha kwa kuwa hawatembei mbali kutafuta maji.”

Matukio ya ukahaba na utumikishaji wa watoto huripotiwa sana katika eneo la njia kuu ya Nairobi kuelekea Eldoret

Nigeria | Prostituierte
Picha: AFP/P. Utomi Epkei

Salgaa ni eneo lililo kwenye njia kuu ya Nairobi kuelekea Eldoret, ambalo ni kiunganishi cha taifa la Kenya na Uganda, na hutumiwa sana na madereva wa matrela na magari mengine ya uchukuzi. Matukio ya ukahaba na utumikishaji wa watoto huripotiwa sana katika eneo hilo ambalo ni mojawapo ya vituo wanaposimama na kulala wahudumu wa matrela wanapokuwa safarini.

Soma zaidi: Nakuru yapandishwa hadhi na kuwa jiji, lakini nini maana yake?

Simulizi zinazoelezewa ni watoto kutumiwa kuwafanyia kazi wahudumu wa trela waposimama hapa, baadhi wakiingizwa kwenye shughuli za ukahaba na kupachikwa mimba au kuambukizwa magonjwa, hivyo kukatiza ndoto zao za elimu. Grace Njuri mwakilishi wa shirika la World Vision anaeleza namna mradi waliouanzisha wa elimu unavyowafaa watoto hawa.

“Watoto nao shuleni kama alivyotuambia Abigail, sasa wameweza kuzingatia masomo. Shughuli yetu kabisa huwa shughuli ya mtoto.Lakini tunajua mtoto ametoka kwa familia fulani, kwa hivyo lazima tushughulikie hiyo familia kwa njia nyingi zingine.”

Gavana wa kaunti ya Nakuru Lee Kinyanjui anahimiza serikali kuzingatia maswala ya kijamii kwenye bajeti yake ili kuweza kumsaidia zaidi mwananchi.

“Ni muhimu sana kwamba, kando na miradi mikubwa tunayofanya ya miundo mbinu, tuanze kuangazia namna ya kuhakikisha mwananchi ana pesa mfukoni. Zi vipi tutawezakitoa huduma na mikopo kwa wafanyibiashara na sekta kama kilimo.”

Sheria ya ajira nchini Kenya inabainisha kwamba, mtoto aliyechini ya umri wa miaka 16 hawezi kuajiriwa.