1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waingereza waliondoka kwa hiari au walishindwa?

Maja Dreyer4 Septemba 2007

Rais Bush alizuru Irak na wakati huo huo Uingereza imeamua kuondoa majeshi yake kutoka Basra. Basi ni sababu kwa wahariri wa magazeti ya humu nchini kuizingatia hali nchini Iraq.

https://p.dw.com/p/CHRw

Kwanza ni gazeti la “Frankfurter Allgemeine” juu ya jeshi la Uingereza kuondoka kutoka mji wa Basra.

“Hatua hiyo pengine imepangwa na kuandaliwa vizuri. Lakini namna ilivyotekelezwa, yaani wakati wa usiku, ilitoa picha kama si hatua ya jeshi kuliondosha kwa hiari bali kama jeshi limeshindwa.”

Moja kwa moja tuendelee na gazeti la “Neues Deutschland”. Limeandika:

“Bush amefika na Waingereza waliondoka, angalau kutoka mji wa Basra. Siku hiyo ya jana ilikuwa kama ishara. Wakati rais Bush amefanya ziara ya ghafla na kujaribu kuwashawishi wenzake juu ya mafanikio ya mkakati wake wa kijeshi, huko Waingereza kama mshirika muhimu zaidi wa Marekani alijitahidi kuweka picha kwamba kujiondoa Basra si kutokana na kushindwa bali kutokana na mpango maalum.”

Ni gazeti la “Neues Deutschland”. Na ufuatao ni uchambuzi wa mhariri wa “Märkische Oderzeitung” na mjini Potsdam:

“Hatua ya Waingereza ambao walikuwa na mkakati bora kuliko Marekani katika kulisimamia eneo la Kusini mwa Iraq kujiondoa kutoka Basra bila ya kuwepo kwa usalama inaonyesha wazi kuwa hali ni ngumu. Tena kuna wasiwasi mwingi ikiwa jeshi la Iraq lina uwezo wa kuhakikisha usalama pamoja na kujenga mfumo wa usimamizi wa kiserikali. Huenda wakaazi waliwachukia wanajeshi wa kigeni waliovamia nchi yao, lakini polisi na jeshi la Iraq halina nguvu ya kutosha kutuliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.”

Gazeti la “Tageszeitung” linalochapishwa mjini Berlin linaonya kuwa nchi ambayo itanufaika kutokana na Waingereza kujiondoa ni Iran. Mhariri huyu ameandika:

“Wanamgambo wa Kishia wanasubiri tu majeshi ya Uingereza kuondoka ili waweze kudhibiti eneo hilo la Kusini mwa Iraq. Kupitia wanamgambo hao, Iran inazidisha mamlaka yake huko Iraq. Sasa itawekwa wazi kuwa Marekani imefanya kosa kubwa kwa kuiita Iran adui badala ya kuihusisha katika kutafuta suluhisho la kisiasa kwa Iraq.”

Vile vile kutoka Berlin ni gazeti la “Tagesspiegel” ambalo linazingatia ziara fupi ya rais Bush wa Marekani nchini Iraq ambapo alitembelea kituo cha kijeshi cha Marekani.

“Bush kwa kweli hakufika nchini Iraq. Kwanza alikaa tu kwa saa chache alipokuwa njiani kwenda Australia. Na pia hakuondoka kutoka kiwanja cha ndege huko Magharibi mwa Iraq chenye ulinzi mkali.”

Na hatimaye ni uchambuzi wa “Landeszeitung” juu ya hali nchini Iraq:

“Marekani imeshindwa katika vita vya Iraq. Bush amefikia lengo moja tu, yaani jina lake litakuwepo katika vitabu vya historia, lakini atakumbukwa kama rais wa Marekani ambaye badala ya kuweka alama ya demokrasia alianzisha moto mkubwa wa machafuko.”