Waislamu waadhimisha Eid-ul-Fitr
13 Mei 2021Saudi Arabia, ambako ndiko kuliko misikiti miwili mitukufu ya Makkah na Madina, ilitangaza tangu jana kwamba leo utakuwa mwanzo wa siku tatu za Eid, baada ya kukamilisha siku 30 za mfungo.
Nchi nyengine ambazo zinaadhimisha Eid leo ni Qatar, Jordan, Misri, Algeria, Syria, Muungano wa Falme za Kiarabu na Tunisia.
Kwa upande wa Afrika Mashariki, Rwanda na Uganda zinaadhimisha pamoja na sehemu nyengine za ulimwengu hivi leo.
Lakini kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, eid rasmi ya kiserikali ni kesho Ijumaa, kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Kiarabu kama vile Oman.
Kama ilivyokuwa kwa Eid ya mwaka jana, mara hii pia inaadhimishwa huku baadhi ya mataifa yakiendelea kufuata kanuni za kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona.
Miongoni mwao ni Iraq, ambako kiwango cha maambukizo ni cha juu na uchomaji wa chanjo ni wa chini, amri ya kudhibiti shughuli za kawaida za maisha zilitangazwa kuanzia jana Jumatano na itaendelea kwa siku 10 zijazo.
Misri, kwa upande wake, imeamuru maduka kufungwa kuanzia saa 3 usiku hadi tarehe 21 Mei, huku Tunisia ikiweka marufuku ya kutembea ovyo hadi Mei 16.
Hata hivyo, mataifa kama Jordan ambako kiwango cha maambukizo kimepunguwa, yametangaza kulegeza masharti ya kutotoka nje usiku kuanzia leo.
Msamaha kwa wafungwa
Nchini Libya, wafungwa 78 waliokuwa wanamgambo wa Jenerali Khalifa Haftar wameachiliwa huru jana jioni, na kuungana na familia zao kwa ajili ya kuadhimisha sikukuu hivi leo.
Hatua kama hiyo imechukuliwa na kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, ambaye ametangaza msamaha kwa wafungwa 2,187 katika kuadhimisha sikukuu hii ya Eid-ul-Fitr.
Uamuzi kama huo alichukuwa mwezi Machi mwaka huu, ambapo aliwaachia huru wafungwa 1,800 kuadhimisha sikukuu ya madhehebu ya Kishia.
Sikukuu hii inayoashiria mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kawaida inaadhimishwa kwa siku tatu, zinazoitwa Iddi Mosi, Pili na Tatu.
Lakini wakati mataifa hayo yakiadhimisha Eid-ul-Fitr kwa sala, dua, misamaha ya wafungwa na ziara za familia, hali ni tafauti kwenye ulimwengu mwengine wa Kiislamu, ambako mauaji, mabomu, vilio na misiba ndiyo inayohanikiza muda huu wa sikukuu.
Mauaji, mashambulizi ulimwengu wa Kiislamu
Ndivyo hali ilivyo Palestina ambako mashambulizi ya Israel yanaendelea kuangamiza maisha ya makumi ya watu kwenye Ukanda wa Gaza.
Mitaa ya Mji wa Gaza inaripotiwa kugeuzwa vumbi na vifusi, huku watu zaidi ya 60, wakiwemo watoto wadogo na wanawake, wakikatiwa uhai wao.
Maduka ambayo muda huu huwa na shughuli nyingi ni matupu na sauti pekee inayosikika ni ya mabomu na magari ya kubebea wagonjwa yakisafirisha majeruhi na maiti.
Nchini Afghanistan, kundi la Taliban limetangaza siku tatu za kusitisha mapigano kupisha sherehe za Eid, lakini si kabla ya mashambulizi ya siku ya Jumamosi kuwauwa watu wapatao 80, wengi wao wasichana wa skuli.
Taliban inakanusha kuhusika na mashambulizi hayo na imeyalaani vikali, huku Marekani ikisema inashuku yamefanywa na kundi linalopingana na Taliban.
Nchini Niger, taifa linalokaliwa na Waislamu wengi magharibi mwa Afrika, wanamgambo waliwavamia na kuwauwa wanakijiji watano katika jimbo la magharibi la Tillaberi linalopakana na Mali na Burkina Faso.
Mashahidi wanasema washambuliaji waliwasili kwenye kijiji cha Fantio hapo kwa pikipiki na kuanza kuwamiminia watu risasi ovyo.
Wanajeshi kutoka kundi liitwalo G5 Sahel, chenye askari kutoka Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger wametumwa kwenye kijiji hicho na wameombwa kusalia huko hadi msimu wa Eid umalizike.