Wajerumani walioathirika na mafuriko hawafikirii uchaguzi
8 Septemba 2021Nchini Ujerumani, katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokea hivi karibuni, watu wana mambo mengine ya kufikiria kuliko uchaguzi. Wanahitaji suluhisho la matatizo yao baada ya mafuriko ya mwezi Julai katika majimbo ya Rhineland Palatinate na North Rhine-Westphalia.
Alama ya misalaba mitatu iliyochorwa kwa rangi ya kupuliza-ndiyo inayoamua hatma yako. Nyumba zenye alama hii ziko katika mji mdogo wa Altenburg katika bonde la Ahr na ziliharibiwa vibaya na mafuriko kiasi kwamba hazina budi kuvunjwa.
Wafanyakazi wa bomoabomoa tayari wameshazibomoa zaidi ya nyumba 10 na nyumba nyingine 20 zimewekwa alama zikisubiri kubomolewa. Hili si jambo rahisi kwa kijiji ambacho takribani watu 500 pekee waliishi kabla ya mafuriko.
Asilimia 95 ya bonde la Ahr limeharibiwa kabisa
Baadhi yao wanataka kuchelewesha shughuli ya ubomoaji. "Nani ajuaye, kama mtu atapata kibali kipya cha ujenzi mahali hapa" anasema mwanakijiji mmoja. Kwa mtazamo wa mabadiliko ya tabia nchi, huenda pasiwe tena na ruksa ya kujenga karibu na mto. Mara nyingi kumekuwa na mafuriko katika bonde la Ahr, lakini kamwe hayakufika kiasi hiki cha maji kujaa hadi kuona mabati pekee.
Asilimia 95 ya eneo hilo limeharibiwa vibaya ikiwa ni pamoja na makazi ya wazee, shule za msingi na mahali pa kufanyia mazoezi. Matope na mabaki ya nyumba zilizoathiriwa kwa kiasi kikubwa yameshakusanywa na kuwekwa kando lakini maji, nyaya za umeme na mawasiliano bado vimeharibika. Kwa sasa, maji ya kunywa yanatoka kwenye matanki ya plastiki. Siyo rahisi kuzungumza na watu wa eneo hili maana wengi wameathiriwa na walichokipitia. "Jirani yetu amefariki”, anasema mwanamke mmoja huku akitazama nyumba jirani iliyoharibiwa. Hakutaka kuzungumza zaidi ya kutikisa kichwa chake alichokiinamisha.
Kundi la wakaazi wa mji huu mdogo wa Altenburg limesimama kwenye kona ya mtaa mbele ya eneo lililojaa kifusi linaonekana kuzungumza zaidi. Watu wakiwa pembeni ya nyumba zao wanamsubiri Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa jimbo la Rhineland-Palatinate Maria Luise Anna Dreyer anayetaka kazi safi ifanyike. Si kila mmoja anaifurahia ziara hii. Angela Merkel anakaribia kuondoka madarakani, inasemekana hawezi tena kuwasaidia. Annika Gemein, 40 anasema "Ujio huu utafanya tusikilizwe zaidi.” "Hatupaswi kusahaulika.”
Watu wa Altenberg wanataka kurudi kwenye makaazi yao
Annika na dada yake Julia wanataka kuzungumza na Kansela Merkel anasema tunataka ahadi kuwa haijalishi ni kiasi gani nyumba ziko mbali na bonde la Ahr wataendelea kuwa na bima dhidi ya mafuriko. Kampuni ya bima iliwaambia kuwa mikataba yao ingeendelea, lakini ni kwa mwaka mmoja hadi miwili pekee.
Watu wa Altenburg kama ilivyo kwa Annika na Julia wanataka kurejea kwenye makazi yao kwani wanasema familia zao zimekuwa zikiishi eneo hilo vizazi na vizazi. Wanasema kama watahamishwa watakuwa wamepoteza zaidi ya makazi. Ndugu hawa wawili wanasema kuwa kila siku, watu wanapambana na mkanganyiko kati ya hisia na mawazo yao. Je wataweza kuishi Altenburg ama ni hatari kwa baadaye? Hadi sasa ni wachache waliofanya maamuzi.
Waziri mkuu wa jimbo la Rhineland-Palatinate Malu Dreyer baada ya kuitembelea Altenburg anasema, anafahamu wasiwasi wa aina hii. Anasema, kuwa kwenye mkondo wa mafuriko haimaanishi kuwa huwezi tena kuishi mahala hapo, lakini tuna maeneo tofauti ambayo tunasema: Unahitaji mifumo tofauti ya kuzuia mafuriko. Unapaswa kuzilinda nyumba kwa namna tofauti na unapaswa kuwalinda watu vizuri zaidi.