1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wa Cologne wasimama kidete dhidi ya vichwa upara

Hamidou, Oumilkher22 Septemba 2008

Wakaazi wa Cologne na serikali ya mji wao wameandika historia dhidi ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia

https://p.dw.com/p/FMir
Wakaazi wa Cologne waandamana kuwazuwia wenye chuki dhidi ya wageniPicha: AP



Juhudi za Marekani na Ujerumani za kukabiliana na mzozo wa fedha ulimwenguni na shambulio la kigaidi mjini Islamabad nchini Pakistan ni miongoni mwa mada zilizomulikwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.Zaidi ya hayo wahariri wamezungumzia kushindwa kufanyika mhadhara wa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia kutoka Ulaya dhidi ya dini ya kiislam katika jiji la Cologne.



Tuanzie lakini Marekani ambako serikali imetenga dala bilioni mia sabaa kwa lengo la kuuvunja nguvu mzozo mbaya kabisa wa fedha kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo.Mpango huo si wa bure,umelengwa pia kwaajili ya uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani ,linahisi gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG:



"Bila shaka yoyote, mzozo huu unampatia nafasi bora zaidi ya ushindi Barack Obama kuliko John McCain,uchaguzi utakapoitishwa November nne ijayo.Mzozo huo wa fedha umebainisha walakin katika mfumo wa kiuchumi-tena wakati huu ambapo wamarekani wengi  wanahisi, hata kiuchumi nchi yao inakwenda mrama .Na wanaobeba jukumu la hali hiyo sio peke yao wanauchumi ,hata serikali imechangia katika hali hiyo."



 Gazeti linalochapishwa Freiburg,BADISCHE ZEITUNG linanadika



"Ulimwengu wa kiuchumi unahitaji sheria kali zaidi.Na Ujerumani inabidi ishike usukani ili kuondowa shaka shaka za Marekani na Uengereza dhidi ya sheria mpya.Watu wanahitaji kutafakari na kukiri ukweli kwamba masoko ya hisa kazi yake ya kweli ni kusaidia kuhakiki thamani ya uchumi."



Kuhusu shambulio la kigaidi katika hotel ya Marriot mjini Islamabad,gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linaandika:



"Shambulio hilo limepiga katika chembe cha moyo cha Pakistan.Hoteli hiyo ilikua ikiangaliwa kama kitambulisho kikubwa cha maisha ya kimagharibi nchini humo..Ikilindwa vizuri kwasababu maafisa walikua wakihofia huenda ikashambuliwa.Al Qaida na waafuasi wengine wa itikadi kali ya dini ya kiiislam kutoka kila pembe ya dunia wanaotumia nguvu ili kueneza itikadi kali,wako nyuma ya shambulio hilo.Wamelitangaza eneo la Pakistan na Afghanistan kua "uwanja wao wa mapambano"- huko ndiko serikali eti zitakakopinduliwa,nchi kuingia katika mitafaruku na ulimwengu wa magharibi kuaibishwa."


Mada ya mwisho inahusu maandamano ya wakaazi wa jiji la Cologne dhidi ya kile kilichotajwa kua "mkutano mkuu dhidi ya kuenea dini ya kiislam" katika mji wao.Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaandika:


"Kwa wanademokrasia wa kweli mkutano huo mkuu umeingia katika madaftari ya historia kama kishindo kilichopelekea kushindwa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.Ni nadra kuona mji mzima unasimama kidete kuwapinga wenye hisia za chuki dhidi ya wageni..Nadra kuwaona raia wa kawaida,wenye mikahawa na hata madereva wa taxi wakisimama mkono kwa mkono dhidi ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.Lakini kutokana na  wakaazi wa Cologne kuwashinda nguvu na kuwanyamazisha vichwa upara,mtu anaweza kusema demokrasia nayo imeingia dowa kwasababu mkutano wao mkuu umepigwa marufuku.


Gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU linatupia jicho machafuko ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa shoto,maarufu kwa jina "wanaojitegemea"-Gazeti linaendelea kuandika:


"Hakuna anaebisha,maandamano ya amani yalifanikiwa.Lakini hata wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kushoto hatuwataki katika mji wetu-wamejipatia kwa mara nyengine tena uwanja wa kutumia maguvu na kwa namna hiyo kuwachochea wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia."