"Wakati wa vita baridi umekwisha"
20 Machi 2007Washirika wote wanne wa mazungumzo haya mjini Washington walionyesha kuwa wanakubaliana katika masuala haya muhimu. Pamoja na mawaziri Rice na Steinmeier waliohudhuria walikuwa kamishna wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Bibi Benita Ferrero-Waldner na mwanadiplomasia mkuu wa Umoja huu, Bw. Javier Solana.
Waziri Rice wa Marekani alikiri kuwa mpango wa Marekani kujenga mitambo ya kufyetua makombora barani Ulaya umezusha wasiwasi nchini Ujerumani, lakini pande zote mbili zinafanya bidii kuutuliza mvutano huu. Kwa kujenga mtambo huu katika nchi za Poland na Tchechnia, Marekani inataka kujilinda dhidi ya shambulio kutoka Iran. Urusi inapinga mitambo hiyo kwa kuwa inahisi ni tishio dhidi yake, na vile vile wanasiasa wa Ujerumani waliikosoa Marekani.
Akizungumzia suala hilo mjini Washington, waziri wa nje wa Ujerumani Steinmeier alisema: “Matakwa ya Marekani kujilinda dhidi ya makombora ya masafa mrefu ni halali, na inatubidi tuyaheshimu matakwa haya. Kwa upande mwingine nadhani Marekani inafahamu kuwa ikiwa mitambo hiyo inatumika pia dhidi ya Ulaya kutakuwa na mjadala.”
Waziri Condoleezza Rice alisema kuwa tangu mwaka mmoja uliopita Marekani imezungumzia suala hilo na Urusi na imehakikisha kuwa mitambo hiyo hailengi dhidi ya Urusi. Wakati wa vita baridi umekwisha, alisema Bi Rice, lakini alisema: “Tunaishi katika dunia ambako inatubidi kujilinda dhidi ya tishio la kinyuklia kama mashambulio madogo mfano kutoka kwa Iran. Na katika dunia kama hii, mitambo ya kufyetua makombora ambayo itaangamiza tishio hilo dogo ni jambo la kuhakikisha usalama badala ya kuathiri usalama.”
Kuhusiana na serikali mpya ya Palestina, waziri Steinmeier wa Ujerumani alisema kuwa pande nne zinazoshughulikia amani ya Mashariki ya Kati kwanza zitatazama kwa karibu hatua na maamuzi serikali hii itakayoyachukua. Kutokana na hayo Ulaya itaamua ikiwa itaiunga mkono serikali hii au la. Waziri Rice alisisitiza kuwa msingi wa kupatikana kwa makubaliano ya amani ni pande zote mbili kutambuana. Javier Solana wa Umoja wa Ulaya alizungumzia matumaini yake kuwa serikali hii itakubali masharti ya makubaliano ya amani.
Hadi Ulaya itakapochukua uamuzi wake kuhusiana na serikali mpya ya Palestina, itaendeleza msaada wake kwa Wapalestina kwa muda wa miezi mitatu. Ulaya inasaidia kwa kupeleka maji na mafuta Palestina pamoja na msaada kwa watu maskini zaidi.
Kwenye mkutano wao, Marekani na Ulaya zimeamua pia kushirikiana zaidi katika juhudi zao za kulinda mazingira.