Wakaazi wakimbia mapigano katika kitongoji kimoja Haiti
15 Novemba 2024Wakaazi katika mojawapo ya kitongoji cha mji mkuu wa Haiti, hapo jana walilazimika kukimbia mapigano makali kati ya wanachama wa genge la wahalifu na polisi wakati ghasia zikipamba moto na msukosuko wa kisiasa.
Watu walionekana wakipakia magodoro na mali nyingine kwenye magari wakati wakijaribu kukimbia kitongoji cha Solino. Kitongoji hicho ni mojawapo ya maeneo machache katika mji mkuu wa Port-au-Prince ambako muungano wa magenge unaofahamika Viv Ansanm, umekuwa ukipambana vikali na polisi katika siku kadhaa zilizopita.
Soma: Vifo vya genge lenye silaha Haiti vyafikia 109
Ghasia zilizuka katika mji mkuu tangu siku ya Jumapili wakati baraza la mpito la Haiti lililoundwa kurejesha utulivu wa kidemokrasia, lilipomtimua waziri mkuu wa mpito huku kukiwa na mizozo ya kisiasa. Taifa hilo la Karibiani halijafanya uchaguzi tangu mwaka 2016, hasa kutokana na vurugu za magenge ya kihalifu.