1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya kuhusu uamuzi wa mahakama kutupa nje mchakato wa BBI

Wakio Mbogho1 Aprili 2022

Uamuzi wa Mahakama ya Juu nchini Kenya kuukataa mchakato na mpango wa maridhiano ya kisiasa, maarufu kama BBI, ulioasisiwa na Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa hasimu wake mkuu, Raila Odinga umeibua hisia mseto. 

https://p.dw.com/p/49KNp
Kenia Nairobi - Oberster Gerichtshof
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Wakenya kutoka maeneo mbalimbali wametoa hisia mchanganyiko kuhusu maamuzi ya mahakama kuu kutupilia mbali rufaa kuhusu mpango wa maridhiano wa BBI uliolenga kurekebisha sehemu za katiba.

Uamuzi huu unajiri baada ya miaka miwili ya vuta nikuvute kati ya wanaounga mkono mchakato wa BBI na wanaopinga jitihada zozote za kuibadilisha katiba iliyopo ya mwaka 2010.

Viongozi wanaounga mkono mchakato wa BBI chini ya mrengo wa Azimio la Umoja wanasisitiza kwamba BBI itafufuka baada ya mgombeaji wao wa Urais, Raila Odinga, kushinda kwenye uchaguzi ujao.

Hata hivyo, mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto hii leo umetoa tangazo kwamba utawaidhinisha wabunge wanaowaunga mkono kupitisha mswada utakaomtaka Mkaguzi Mkuu wa Fedha nchini, Nancy Gathungu, kuchunguza fedha zilizotumika kwenye mchakato wa kutengeza BBI.

Jaji Mkuu nchini Kenya Martha Koome.
Jaji Mkuu nchini Kenya Martha Koome.Picha: JUDICIAL SERVICE COMMISSION/REUTERS

Wachambuzi wanauelezea uamuzi huu wa mahakama kama dhihirisho tosha la uhuru wa mahakama, ambacho ni kigezo muhimu taifa hili linapoelekea kwa uchaguzi mkuu chini ya miezi mitano ijayo.

Hakimu Joel Ngugi wa mahakama ya juu, ambaye aliongoza jopo la majaji waliotoa hukumu ya kwanza dhidi ya BBI mwaka uliopita, kabla ya uamuzi huo kutolewa rufaa, anasema mahakama iko imara na tayari kwa uchaguzi mkuu ujao. Amepigia upatu mbinu ya kutafuta njia mbadala kusuluhisha mizozo ya uchaguzi:

"Wakati kesi zinapoletwa mahakamani kile tunachofanya ni kutangaza nani ameshinda na nani hajashinda, hili halisuluhishi malalamiko au matatizo yalioko. Lakini huu mfumo mbadala unawapa washirika nafasi kuangazia matatizo haya na kwa usaidizi wa wapatanishi wanaweza kurejesha mahusiano yaliyokuwa yamepotea.”

Naibu jaji mkuu nchini Kenya Philomena Mwilu.
Naibu jaji mkuu nchini Kenya Philomena Mwilu.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Mahakama imeunda kamati maalum inayoyajumuisha mashirika ya kijamii, maafisa wa polisi, magereza kati ya wadau wengine kuangazia maswala wanayohishi yanakuwa vikwazo kwa wananchi kufikia haki. Cornelius Oduor, afisa mkuu katika shirika la kijamii linaloshughulikia uongozi bora, CEDGG.

"Uzembe ambao ulikuwa hapo awali, ukosefu wa mawasiliano, kupotea kwa ushahidi, kesi kuchukua muda mrefu; yote haya yanapata kuangaziwa,” amesema Oduor.

Kadhalika, kufuatia maamuzi kuhusu mpango wa BBI, Jaji Mkuu Martha Koome ametoa onyo kwa mawakili dhidi ya kutumia mitandao ya kijamii kujaribu kushawishi uamuzi wa mahakama.

Je ni kweli mahakama ya Kenya inasadifu kuitwa chombo huru?