1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wakumbuka miaka 20 ya mashambulizi ya al-Qaida

Shisia Wasilwa
6 Agosti 2018

Miaka 20 baada ya mashambulizi ya kigaidi kuuwa zaidi ya watu 100 na kujeruhi wengine kadhaa kwenye ubalozi wa Marekani nchini Kenya, bado waathiriwa wanasaka fidia kutoka kwa serikali ya Marekani - na hawajafanikiwa.

https://p.dw.com/p/32h0h
Kenia Anschlag US Botschaft 1998
Picha: AP

Tarehe 7 Agosti 1998, saa 4:00 asubuhi, John Ngige alikuwa anatembea karibu na ubalozi wa Marekani jijini Nairobi akielekea kwenye duka la fundi wa vidio. Hakuwa na habari kuwa shambulizi lililofanywa na kundi la kigaidi la al-Qaida lingeyabadilisha maisha yake milele, kwani mripuko huo umemuachia John kovu la ulemavu.

John ndiye mwenyekiti wa chama cha wahanga wa mripuko huo na anaikumbuka siku hiyo kama kwamba ilikuwa jana. 

John, ambaye sasa anatembea kwa kutumia fimbo, anasema kuwa ni mmoja kati ya waathiriwa wapatao 1,000 ambao wamekuwa wakigharamia matibabu yao wenyewe.

Lakini hadi sasa angali anamatumaini kuwa Marekani itawafidia na kumpunguzia mzigo wa gharama za matibabu, licha ya kusema kwamba "uamuzi wa mahakama katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukiwapuuza waathiriwa wa Kenya kutokana na majeruhi waliyopata."

Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) lilitoa fidia ya dola milioni 45 sawa na shilingi bilioni 4.5 kwa familia 173 za Wakenya waliouawa ama kujeruhiwa kwenye mripuko huo wa Agosti 7. Lakini waliofidiwa ni wale tu waliokuwa wanahudumu katika ubalozi huo.

Malalamiko mbele ya Congress

Somalia USA Fahndungsplakat von Al-Qaida Terroristen
Tangazo la kumsaka mmoja wa washukiwa wakuu wa mashambulizi hayo ya Nairobi, Fazul Abdullah Mohammed.Picha: AP

Juhudi za wanaharakati kama John Ngige sasa zinalenga bunge la Congress la Marekani. Wanalenga kushawishi wabunge kurekebisha sheria iliyopitishwa mwaka 2015, ambayo inaeleza kuwa fidia inastahili kutolewa kwa raia wa Marekani pekee. Marekebisho kwenye sheria hiyo yakifanikiwa, yatawasaidia waathiriwa wa mlipuko huo kufidiwa. 

Ngige anasema kuwa kwa sasa zaidi ya wahanga 350 wa mripuko huo wametia saini ombi la kufika mahakamani wakitaka kushinikiza serikali za Kenya na Marekani kuwapa fidia kwa majeraha na hasara walizopata. 

Mnamo Agosti 2014, mahakama moja ya New York nchini Marekani iliwapa fidia ya shilingi bilioni 100 sawa na dola bilioni moja Wakenya sita waliojeruhiwa kwenye mripuko huo.

Hata hivyo, mahakama hiyo iliongeza kusema kuwa watapewa fedha hizo punde mali ya kundi la al-Qaida itakapopatikana na kuuzwa. 

Leo hii, wakati wahanga wa mripuko huo wanapokumbuka miaka 20 ya siku iliyoyabadilisha maisha yao milele, wanatumai kuwa machozi yao ya muda mrefu yatapanguswa na serikali ya Marekani kwani wanahoji kuwa, serikali hiyo ilistahili kuwajibika kwa usalama wa ubalozi huo.

Mwandisgi: Shisia Wasilwa/DW Nairobi
Mhariri: Daniel Gakuba