1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi kutoka Syria wamiminika kuelekea Uturuki

Admin.WagnerD5 Februari 2016

Maelfu ya wakimbizi kutoka Syria wanaripotiwa kumiminika kuelekea nchini Uturuki, katika wimbi jipya lililosababishwa na kusonga mbele kwa vikosi vya serikali dhidi ya waasi.

https://p.dw.com/p/1HqFq
Wakimbizi kutoka nchini Syria.
Wakimbizi kutoka nchini Syria.Picha: picture alliance/AA/A. Muhammed Ali

Hatua hii inakuja mnamo wakati washiriki katika mkutano huo uliokuwa na lengo la kuchangia fedha kwa ajili ya kukabiliana na matataizo yanayoyasababishwa na mgogoro huo, wakisema jitihada za kumaliza mgogoro huo hadi sasa hazionyeshi matumaini yoyote ya kuzaa matunda,kutokana na kuongezeka kwa mapigano nchini Syria siku hadi siku, kuahirishwa kwa mazungumzo ya amani mara kwa mara, kushindwa kukubaliana kwa mataifa ya Urusi na nchi za magharibi kuhusiana na jinsi ya kuutatua mzozo huo wa Syria huku mamilioni ya raia wa Syria wakiendelea kushuhudia mashambulizi ya anga, kukosa makazi na pia kukabiliwa na njaa.

" Hali nchini Syria kwa sasa ni mbaya zaidi " alisikika akisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

USA Kerry beim IS Außenministertreffen in Rom
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John KerryPicha: Reuters/N. Kamm

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alisema baada ya kipindi cha karibu miaka mitano ya mapigano nchini Syria , hali bado si ya kuridhisha nchini humo na inazidi kuwa mbaya.

Mkutano huo wa siku moja ulilenga kuboresha jitihada za kujaribu kusaidia watu karibu ya milioni 4.6 ambao tayari wamekimbia mapigano yanayoendelea nchini Syria na kutafuta hifadhi katika nchi jirani za Jordan, Lebanon na Uturuki. Watu wengine milioni sita au zaidi wameyahama makazi yao ndani ya Syria.Wengine zaidi ya robo milioni wamepoteza maisha yao.

Ahadi ya fungu hilo la fedha zilizoahidiwa katika mkutano huo zinalenga pia kusaidia kupunguza idadi ya watu wanaokimbia nchi hiyo kutokana na hali mbaya ya maisha kwa kuandaa mazingira bora ya utoaji elimu, upatikanaji wa ajira kwa wakimbizi kutoka nchini Syria walioko katika mataifa ya Mashariki ya Kati na pia kuziwezesha kiuchumi nchi zinazolemewa na mzigo wa kuwapokea wakimbizi.

David Cameron asema fedha zote kupatikana ifikapo mwaka 2020

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, alisema washiriki wa mkutano huo ulioratibiwa kwa pamoja na mataifa ya Uingereza, Ujerumani, Norway, Kuwat na Umoja wa Mataifa tayari walikuwa wameahidi kiasi cha karibu dola bilioni 6, kwa mwaka 2016 na kiasi kingine cha fedha dola bilioni 5 kuwa kimepatikana ifikapo mwaka 2020.

Baadhi ya viongozi walioshiriki mkutano wa London.
Baadhi ya viongozi walioshiriki mkutano wa London.Picha: Reuters/A. Rain

Kwa upande mwingine mashirika ya misaada ya kimataifa yalionyesha kupongeza msaada huo wa fedha, lakini pia yakailaumu jumuiya ya kimataifa kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti za kumaliza vita inayoendelea nchini Syria.

Wakati huohuo maelfu ya raia wa Syria hii leo walikuwa wakiendelea kumiminika kuelekea nchini Uturuki mnamo wakati vikosi vya serikali ya Syria kwa msaada wa Urusi vikizidisha mashambulizi katika maeneo yanayozunguka Aleppo huku Uturuki na Urusi zikiendelea kushutumiana kutokana na kuendelea kukua kwa mgogoro huo.

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davotoglu akizungumza katika mkutano huo wa London alisema kiasi cha watu 70,000 walikuwa wakielekea nchini Uturuki wakikimbia mapigano nchini Syria.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri : Daniel Gakuba