1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi waongezeka duniani

20 Juni 2018

Ripoti ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, inaonesha kuwa idadi ya wakimbizi duniani ni kubwa zaidi kuliko raia wote wa Ufaransa na Uingereza wakichanganywa pamoja.

https://p.dw.com/p/2zuS2
Tansania Weltflüchtlingstag 2018
Picha: DW/Prosper Kwigize

Daima dunia imekuwa ikishuhudia watu wanaolazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na vita, mashambulizi au sababu nyenginezo. Lakini kwa sasa hali inazidi kuwa mbaya. Kwa ujumla, mwaka uliopita pekee, watu milioni 68 na nusu walijikuta ukimbizini, likiwa ongezeko la watu milioni tatu ikilinganishwa na mwaka juzi. Hivyo ndivyo zilivyo hesabu, kwa mujibu wa Kamishna wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Bwana Filippo Grandi.

"Hiyo ni ishara mbaya, kwa kuwa tayari idadi ya wakimbizi ilishakuwa kubwa sana, na sasa imeongezeka tena. Hili linamaanisha kitu kimoja. Kwamba migogoro, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha wakimbizi, haiweza kutatuliwa. Kwa hakika, tunaishi kwenye dunia iliyoshindwa kuleta amani," anasema Kamishna Grandi.

Ongezeko hili la wakimbizi kwa mwaka uliopita linahusishwa na mizozo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, vita vya Sudan Kusini na jaala ya maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia Bangladesh kutokea Myanmar.

Takwimu za wakimbizi duniani

Tansania Weltflüchtlingstag 2018
Mtoto kwenye kambi ya wakimbizi nchini Tanzania, akiwa sehemu ya wakimbizi 355,000 kutoka Kongo na Burundi.Picha: DW/Prosper Kwigize

Robo tatu ya wakimbi wanatokea kwenye mataifa matano tu: Syria, Afghanistan, Sudan Kusini, Myanmar na Somalia. Laiti angalau nchi moja kati ya hizi inafanikiwa kumaliza mizozo yake, basi taswira ya jumla ya idadi ya wakimbizi duniani nayo ingebadilika.

Wengi wa wakimbizi, hata hivyo, ni wale wanaokimbilia upande mwengine wa nchi yao, wakikimbia upande wenye machafuko, yaani wakimbizi wa ndani.

Na wengi wa wale wanaokimbilia nje ya nchi yao, basi hukimbilia kwenye mataifa yaliyo jirani. Kwa mfano, Uturuki inahifadhi hivi sasa wakimbizi milioni 3 unusu kutoka Syria, hali inayoifanya kuwa nchi iliyopokea idadi kubwa kabisa ya wakimbizi duniani.

Hata hivyo, kwa sababu ya idadi ya raia wake wenyewe, ni Lebanon ndilo taifa lililoelemewa zaidi na mzigo wa wakimbizi. 

Filippo Grandi anaangalia suala la ufunguaji mipaka kwa kila mtu anayetaka hifadhi ya kimataifa kuwa la muhimu sana.

Kitisho cha mataifa kufunga mipaka kuwazuwia wakimbizi

Deutschland Berlin - Angela Merkel, Filippo Grandi und William Lacy Swing
Kamishna wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, Filippo Grandi, akiwa na Kansela Angela Merkel mjini Berlin mwaka 2017.Picha: picture alliance/dpa/AA/M. Gambarini

Kamishna huyo wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa anautazama mjadala wa mataifa ya Ulaya juu ya ufungaji mipaka na kuimarisha taratibu za kuwashughulikia wakimbizi kwa wasiwasi mkubwa.

"Tunaamini kuwa Ulaya inapaswa kuendelea kuwa kigezo chema cha kuwapokea waomba hifadhi kama ambavyo imekuwa kwa miongo kadhaa sasa. Kwa sababu, natuwe wa kweli, kama Ulaya ikifunga milango yake, tunawezaje kuyashawishi mataifa masikini ya Afrika, Mashariki ya Kati, Asia na Amerika Kusini kufungua mipaka yao kwa watu wanaokimbia mizozo mibaya kabisa kwenye nchi zao?", anahoji Kamnishna Grandi.

Ingawa idadi ya wakimbizi duniani inazidi kuongezeka, wale wanaokimbia Ulaya wanazidi kupungua, hata kwa taifa kama Ujerumani ambalo liliwahi kuongoza kampeni ya kuwapokea waomba hifadhi.

Mwaka jana, ni waomba hifadhi 187,000 tu waliongia hapa, wakati mwaka 2015, idadi ilikuwa mara tano zaidi. Filippo Grandi anaiomba Ujerumani kuendelea kuwa shujaa wa ubinaadamu.

"Tunatarajia sana Ujerumani itaendelea kuliongoza bara la Ulaya katika kutekeleza sera ya pamoja ya wakimbizi na wahamiaji. Mijadala mingi inaendelea huku ikiingizwa siasa ndani yake, lakini ni muhimu kwa serikali hii ya Ujerumani na yoyote ijayo, kuendelea kuheshimu maadili haya."

Kamishna huyo wa wakimbizi anayatolea wito mataifa yote kutoacha kuwasaidia wale waliokimbia makwao, akisema kuwa "hakuna mtu ambaye anakwenda ukimbizini kwa hiyari yake, lakini sisi tunaweza kuwasaidia watu hawa kwa hiyari yetu."

Mwandishi: Mäurer, Dietrich Karl (SWR Zürich) 
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf