1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakongo hawajafikiwa na misaada licha ya usitishwaji vita

12 Julai 2024

Licha ya kusitishwa kwa vita kwa muda wa wiki mbili kuanzia Julai 5, shughuli za kutoa msaada wa kibinadamu bado hazijafanyika katika maeneo yote yaliyoathirika, jambo ambalo linawasikitisha wakaazi wa maeneo hayo.

https://p.dw.com/p/4iDlu
Watu wamekusanyika pembezoni mwa tukio la mlipuko katika kambi ya wakimbizi nje kidogo ya mji wa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Watu wamekusanyika pembezoni mwa tukio la mlipuko katika kambi ya wakimbizi nje kidogo ya mji wa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Tangu kuanza kwa kusitishwa kwa vita, mashirika ya kibinadamu bado hayajapelekwa kwenye maeneo ya vita kwa hofu ya kukiukwa kwa usitishaji wa mapigano kati ya pande zinazopigana.

Ingawa serikali za Kongo na Rwanda zimetangaza kuunga mkono usitishaji wa vita wa kibinadamu kwa wiki mbili ili kupunguza mateso ya watu wanaoishi katika hali ngumu na kuweka mazingira ya kupunguza mvutano zaidi mashariki mwa Kongo, ukiukaji wa mpango huo unatokea katika eneo la Masisi, na mapigano katika vijiji vya Nyange na Bibwa katika kikundi cha Bashali Mokoto.

Jana, Alhamisi, waasi walichukua udhibiti wa vijiji kadhaa vikiwemo Nyange, Mukengwa na Bibwe.

Soma pia: UN yaishtumu Uganda kuwasaidia waasi wa M23

Kulingana na mkuu wa ofisi ndogo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashugulikia Wakimbizi - UNHCR huko Goma, hali kama hii inaonesha ni kwa nini mashirika ya kibinadamu yanashindwa kutuma maafisa wao katika maeneo hayo.

Abdoulaye Barry, amesema, "Kwetu sisi, tunajaribu kuona na kutafiti hatua zinazowezekana za kufikia maeneo husika, lakini usalama wa wafanyakazi wa kibinadamu ni muhimu sana. Ndiyo maana inapotokea kuwa ni maeneo ya mapigano na maisha ya wafanyakazi yako hatarini, tunapendelea wafanyakazi wakae wakisubiri hali itulie."

DR Kongo Kibumba 2022 | Waasi wa M23
Waasi wa M23 wakishika doria huko Kibumba, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Desemba 23, 2022.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Wakazi wa maeneo yaliyoathirika wanajiuliza: mkataba wa kusitisha mapigano kwa lengo la kurahisisha usambazaji wa msaada wa kiutu, una faida gani ikiwa msaada wa kibinadamu hauwezi kuwafikia?

Mkazi mmoja wa Kanyabayonga aliyehojiwa na DW kwa kuficha jina lake, anayaomba mashirika ya kibinadamu kutumia fursa hii haraka, kwa sababu watu wanateseka katika maeneo haya.

Soma pia: Baraza la Usalama laonya dhidi ya hali mbaya Kongo

 "Wakati wa mapigano, mashirika mengi ya kibinadamu yaliondoka katika maeneo yetu. Tangu kuanza kwa kusitishwa kwa vita kwa madai ya kibinadamu, hakuna hata mmoja wao aliyerudi kusaidia wakimbizi wa ndani na wale waliorejea. Mashirika ya kibinadamu ya tumia nafasi hii haraka ili kuwaletea msaada wanaohitaji."

utulivu wa muda kaskazini mwa mkoa wa Kivu Kaskazini, hususan katika wilaya za Lubero na Rutshuru, umewezesha wakazi wengi waliokimbia makazi yao kurudi vijijini kwao. Kwa wakati huu, wakazi wanaendelea kuishi katika hali duni, wakitumaini kuwa usitishaji wa mapigano utaleta msaada wanaohitaji kwa dharura.