Wakorea kusini wakutana na Wakorea kaskazini
20 Agosti 2018Tukio hilo litakalodumu kwa muda wa wiki moja katika mji wa kitalii ulioko katika milima ya Diamond nchini Korea kaskazini linakuja wakati Korea hizo mbili zinaimarisha juhudi za maridhiano huku kukiwa na msukumo wa kidiplomasia kutatua mkwamo wao kuhusiana na azma ya Korea kaskazini ya mpango wake wa silaha za kinyuklia ambao unaweza kushambulia bara la Amarika.
Kukutana huko kwa muda kwa ndugu kutoka pande hizo mbili kunaonekana kuwa na hisia kali kwasababu washiriki wengi ni wazee na wana haja ya kuwaona wapendwa wao kwa mara nyingine tena kabla hawajafariki. Familia nyingi zimegawika wakati wa vita vya Korea vya mwaka 1950-53, ambavyo vilimalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano , na sio mkataba wa amani, na kuliacha eneo la rasi ya Korea kiufundi katika hali ya vita.
Mabasi yaliyowabeba kiasi ya wazee 90 kutoka Korea kusini pamoja na wanafamilia wengine yaliingia katika mji huo wa kitalii wa milima ya Diamond baada ya kuvuka kuingia nchini Korea kaskazini. Hapo mapema asubuhi, Wakorea kusini , baadhi wakiwa katika viti vya kusukuma na wakisaidiwa na wafanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu , waliyaacha mabasi kwa muda na kuingia katika ofisi za uhamiaji za Korea kusini katika mji wa mpakani wa mashariki wa Goseong.
Walikuwa wanakutana tena leo mchana na ndugu zao wa Korea kaskazini ambao walipoteana kwa muda mrefu mwanzoni mwa tukio hilo la siku tatu. Duru nyingine ya kukutana kuanzia Ijumaa hadi Jumapili itahusisha zaidi ya Wakorea kusini 300, kwa mujibu wa wizara ya muungano ya mjini Seoul.
Wakimbizi wa vita
Makutano yaliyopita yametoa picha nzuri za wazee Wakorea wakilia, wakikumbatiana na kuonesha mapenzi makubwa kwa kila mmoja. Karibu watu 20,000 wamekuwa wakishiriki katika duru 20 za kukutana uso kwa uso tangu mwaka 2000.
Wengine 3,700 walibadilishana ujumbe wa vidio na ndugu zao wa Korea kaskazini chini ya mpango huo unaodumu kwa muda mfupi kuanzia mwaka 2005 hadi 2007.
Hakuna aliyewahi kupata nafasi ya pili kuwaona ndugu. Wengi wa washiriki kutoka Korea kusini ni wakimbizi wa vita waliozaliwa nchini Korea kaskazini ambao watakutana na ndugu zao , ama watoto wao waliokuwa wadogo waliobakia nchini humo, wengi wao ambao sasa wamo katika umri wa miaka ya 70.
Park Hong-seo , mwenye umri wa miaka 88 ambaye alipigana vita vya Korea kutoka mji wa kusini wa Daegu, amesema anawaza kila mara iwapo alikabiliana na kaka yake mkubwa katika mapambano.
China yaingilia kati
Baada ya kumaliza masomo yake katika chuo kikuu cha mjini Seoul, kaka yake Park alikwenda kuishi katika mji wa pwani wa Korea kaskazini wa Wonsan akifanyakazi kama daktari wa meno mwaka 1946.
Baada ya vita kuzuka, Park aliambiwa na mfanyakazi mwenzake kuwa kaka yake amekataa kukimbilia Korea kusini kwasababu alikuwa na familia upande wa kaskazini na ni daktari katika jeshi la Korea kaskazini.
Park alipigana upande wa Korea kusini akiwa mwanafunzi mwanajeshi na alikuwa miongoni mwa vikosi vya muungano ambavyo viliukamata mji wa Wonsan Oktoba mwaka 1950. Majeshi yaliyokuwa yakiongozwa na Marekani yalisonga mbele zaidi upande wa kaskazini katika wiki zilizofuata kabla ya kufurushwa kurejea nyuma na majeshi ya China baada ya Beijing kuingilia kati katika mzozo huo.
Park alikuja kufahamu kwamba kaka yake alifariki mwaka 1984. Katika mlima Diamond atakutana na watoto wa kiume na kike wa kaka yake kutoka Korea kaskazini ambao sasa wana umri wa miaka 74 na 69.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman