Wakurdi wa Afrin waomba msaada kijeshi wa Syria
26 Januari 2018Maafisa wa Kikurdi katika mkoa wa Afrin katika taarifa yao wametoa mwito kwa serikali ya Syria kutekeleza wajibu wao wa kulinda mipaka ya nchi hiyo dhidi ya mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya Uturuki.
Mwenyekiti mwenza wa baraza la mji wa Afrin Othiman Al -Sheikh Issa alilieleza shirika la habari la AFP kuwa Rais wa Syria Bashar al-Assad anapaswa kuingilia kati hali hii na kutoruhusu ndege za Uturuki kuruka katika anga ya Syria.
Alisema wana amini kuwa Afrin ni sehemu ya Syria na kuwa shambulizi lolote dhidi ya Afrin ni shambulizi kwa watu wa Syria pamoja na uchokozi dhidi ya taifa hilo.
Operesheni hii ya Uturuki katika jimbo la Afrin inaonekana kuwa changamoto kubwa kwa wakurdi katika juhudi zao za muda mrefu za kutaka kuwa na taifa lao likijumuisha wakurdi walioko Uturuki na Kaskazini mwa Syria.
Uturuki ilianzisha mashambulizi mpakani mwa Syria Jumamosi iliyopita dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi wenye mafungamano na kundi la YPG ambalo Uturuki inalichukulia kama kundi la kigaidi.
Haya yanajiri mnamo wakati Uturuki kupitia kwa msemaji wa rais Recep Tayyip Erdogan ikitoa mwito kwa Marekani kusitisha uungaji wake mkono kwa wapiganaji wa wakikurdi wa YPG vinginevyo iwe tayari kukabiliana na vikosi vya Uturuki katika mapiagano ya ardhini nchini Syria.
Marekani yasema inafuatilia silaha zinazotumiwa na YPG
Nayo wizara ya ulinzi ya Marekani imesema inafuatilia kwa makini silaha zinazotumiwa na YPG ili zisije kuangukia katika mikono isiyo salama na kuwa Marekani itaendelea pia na mashauriano na Uturuki.
Marekani imekuwa ikiwaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi wa YPG kaskazini mwa Syria katika mapambano dhidi ya kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu hatua ambayo imekuwa haiifurahishi Uturuki.
Tofauti na Marekani, Uturuki inasisitiza kuwa YPG wanamafungamano na chama cha wafanyakazi kilichopigwa marufuku cha PKK.
Waziri wa Uturuki anayehusika na masuala ya ulaya Omer Celik amelieleza shirika la habari la AFP kuwa operesheni hiyo kaskazini mwa Syria inalenga kulinda masilahi ya kiusalama ya Uturuki na pia kulinda usalama wa ulaya.
Akizungumza hapo jana Alhamisi mjini Brusssels waziri huyo alisema tayari walikwishawaeleza bayana marafiki na washirika wao juu ya haja ya kutowaunga mkono wapiganaji wa YPG na kuwa wanapaswa kushirikiana katika operesheni hiyo lakini badala yake hawakufanya hivyo na ndio sababu Uturuki ikaamua kuanzisha mashambulizi.
Ingawa rais wa Syria Bashar Assad anaonekana kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa Uturuki katika ukanda huo bado kuna mashaka iwapo kiongozi huyo ataitikia wito wa maafisa wa Kikurdi.
Rais Assad mara kadhaa amekuwa akipinga wazo la wakurdi kutaka kuwa na taifa lao na katika siku zilizopita amewahi kutishia kuwasambaratisha wale anaowaita wasaliti wa Syria.
Uturuki pia inasisitiza kuwa ilifikia makubaliano na Urusi ambayo ni mshirika mkuu wa rais Bashar Assad kabla ya kuanzisha mashambulizi hayo nchini Syria.
Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe
Mhariri: Caro Robi