Wakurdi wa Iraq wajianda na kura ya kujitenga
24 Septemba 2017Serikali kuu mjini Baghdad imeitaja kura hiyo kuwa inayokiuka katiba. Kuna wasiwasi kwamba kura hiyo huenda ikasababisha machafuko, na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yametaka iahirishishwe au kufutwa kabisaa, wakisema itatatiza vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu.
Katika mji mkuu wa jimbo hilo wa Arbil, ambao ni ngome ya kisiasa ya rais Massud Barzani alieasisi kura hiyo ya maoni, bendera za Kikurd zilikuwa zinapepea kila mahala.
"Tunasubiri kusikia hali itakavyokuwa baada ya Septemba 25, kwa sababu Wakurdi wengi zaidi watapigakura kuchagua uhuru ili kutimiza ndoto yetu ya kuwa na taifa huru," alisema kibarua Ahmad Souleiman mwenye umri wa miaka 30. "Tunachohofia ni kwamba maadui zetu wana nia mbaya na sisi," aliongeza.
Iran na Uturuki zina idadi kubwa ya Wakurd wao na zinahofia kura hiyo itachochea hisia za kujitenga nyumbani.
Kura yawaunganisha maadui
Karibu Wakurd milioni 5.5 wanatarajiwa kupiga kura katika mikoa mitatu ambayo tangu mwaka 2003, imeunda jimbo huru la Wakurdi lakini pia katika maeneo yanayozozaniwa na serikali ya mjini Baghdad, kama vile mkoa wenye utajiri wa mafuta wa Kirkuk.
"Sote tunaunga mkono uhuru kwa sababu hatuoni manufaa ya kubakia nchini Iraq. Lakini tunaogopa njama za mataifa jirani," alisema Kamaran Mohammed, muuza nguo mwenye umri wa miaka 27 mjini Arbil. "Leo tunaona mataifa jirani yakiweka kando tofauti zao kuungana dhidi yetu."
Siku ya Jumamosi, waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim alionya kuwa hatua za Ankara kujibu kura hiyo ya maoni zitakuwa na "muelekeo wa kiuchumi na kiuslama." Alipoulizwa iwapo operesheni za kuvuka mipaka za kijeshi zitakuwa mmoja ya uwezekano, Yildirim alisema "bila shaka", lakini hilo ni suala la muda wa lini njia ya kiusalama, kiuchumi na kisiasa zitatumiwa."
Vyama vya Kikurd vyatofautiana
Wakati taifa huru limekuwa ndoto ya Wakurd walioko nje, vyama vikuu viwili vya kundi hilo la kikabila nchini Iraq vinatofautiana juu ya namna yakufanikisha jambo hilo. Chama cha Barzani cha Kurdistan Democratic Party (KDP) na Patriotic Union of Kurdistan (PUK) chake Jalal Talabani viko pande mbili tofauti kisiasa kuhusu suala hilo.
Mudah Bakhtiar wa kamati ya kisiasa ya PUK alisema siku ya Jumamosi kwamba chama chake "kinaamini kwamba mpango mbadala kwa kura ya maoni uliopendekezwa na Umoja wa Mataifa na mataifa makubwa unakubalika."
Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yanaunga mkono mpango "mbadala" wa kuwepo na majadiliano ya mara moja kuhusu uhusiano wa baadae ili kuachana na kura ya maoni. Mjini Sulaymaniyah, mjini wa pili unaodhibitiwa na PUK katika jimbo hilo huru, shauku ya kura hiyo imepungua.
Hama Rashid Hassan mwenye umri wa miaka 51, alikwenda katika kituo cha kupigia kura siku yay Jumapili kuhakiki jina lake kwenye orodha ya wapigakura. "Tangu nikiwa mtoto, Nimekuwa na ndoto ya siku moja bendera yetu kupepea katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa," alisema.
Lakini wapigakura wengine wanachukua tahadhari zaidi. "Nitapiga kura ya 'hapana', kwa sababu nahofia vikwazo dhidi ya jimbo letu, vita vya wenyewe kwa wenyewe na wanamgambo wa Kishia wa Hashed al-Shaabi, na kuamka siku moja na kuona wanajeshi wa Uturuki wakipiga doria," alisema mwalimu Kamiran Anwar mwenye umri wa miaka 30.
Eneo nyeti zaidi ni Kirkuk ambako watu walikimbilia kununua hifadhi ya chakula siku ya Jumamosi kujiandaa na matatizo yanayoweza kufuatia kura ya maoni. Mbunge Alaa Talabani alisema kungekuwa na mkutano mjini Arbil Jumapili jioni kuhusu kuahirisha kura mjini Kirkuk.
Wanamgambo wa Kishia watishia kuwadhibu waandaji
Mkoa wa Kirkuk, ambao ni nyumbani kwa Wakurd, Waarabu na Waturkmen, unazozaniwa kati ya serikali kuu mjini Baghdad na Wakurd wa nchi hiyo. Wakurd wanasema mkoa huo ni wa kwao kihistoria, wakihoji kwamba kiongozi wa zamani Saddam Hussein aliwatimua katika mkoa huo na nafasi yao kuchukuliwa na Waarabu.
" Kutakuwa na ghara kubwa ya kulipwa na walioandaa kura ya hii ya maoni, uchokozi unaolenga kuharibu uhusiano kati ya Waarabu na Wakurd," alisema kiongozi wa kundi la Hashed al-Shaabi Faleh al-Fayad. "Mara tu kura ya maoni itakapofanyika kutakuwa na hatua za kisheria na kikatiba."
Kundi la wanamgambo wa Hashed liliundwa mwaka 2014 kupambana dhidi ya kundi la Sola la Kiislamu IS. Kundi la mgambo linaloungwa mkono na Iran, linalokuja chini ya mwavuli wa Hashed, liliweka wazi msimamo wake wa upinzani dhidi ya kura ya maoni.
Msemaji wake alizitaka mamlaka za serikali kuu "kuchukua hatua kukabiliana na mradi huu unaotishia amani ya kiraia na usalama wa taifa."
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Saumu Yusuf