1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa G7 wawasili Hiroshima tayari kwa mkutano wa kilele

18 Mei 2023

Rais Joe Biden wa Marekani amekutana na waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida mchana wa leo baada ya kuwasili nchini humo tayari kushiriki mkutano wa kilele wa kundi la mataifa tajiri ulimwenguni la G7.

https://p.dw.com/p/4RXqA
Japan | G7-Gipfel in Hiroshima
Picha: Kiyoshi Ota/REUTERS

Kwenye mazungumzo kati ya rais Joe Biden na waziri mkuu wa Japan, Fumio Kishida, walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi na kuzikabili tabia za uchokozi za China. 

Hivyo ndivyo waziri mkuu Fumio Kishida wa Japan alivyoanzisha safari ya mkutano huo wa kilele, baada tu ya rais Joe Biden kuwasili katika kambi ya kijeshi karibu na mji wa Hiroshima mapema leo.

Kishida ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo alirudia matamshi yake kwamba mahusiano kati ya Japan na Marekani ndio kiini ama msingi wa amani na utulivu katika kanda ya bahari ya Hindi na Pasifiki na kuongeza kuwa anatumai kwenye mkutano huo wa Hiroshima, watadhihirisha azma isiyotetereka ya G7 ya kuendeleza utaratibu ulio huru na wazi wa kimataifa unaozingatia utawala wa sheria.

Rais Joe Biden kwa upande wake amemwambia Kishida kwamba mataifa hayo mawili kwa pamoja watamwajibisha Urusi kutokana na hatua yake ya kuivamia Ukraine kwa kuwa kwa pamoja wanasimamia maadili yanayofanana katika mazingira ya sasa yanayokabiliwa na kitisho cha kiusalama na hasa kwa watu wa Ukraine.

"Kama ulivyosema, mwezi Januari, ulipokuwa Ikulu.. nadhani ulisema 'tunakabiliwa na moja ya mazingira magumu zaidi katika historia ya hivi karibuni. Na unajua, tunasimamia maadili ya pamoja, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono watu jasiri wa Ukraine wanapotetea eneo lao huru, na kuiwajibisha Urusi kwa uchokozi wake,” alisema Biden.

Logo ya mkutano wa G7 uliowakutanisha mawaziri wa fedha wa mataifa wanachama kabla ya mkutano wa kilele unaoanza Ijumaa, 19.05.2023.
Picha: Issei Kato/REUTERS

Biden amekutana na Kishida kabla ya mkutano huo wa kilele wa G7 utakaoanza kesho Ijumaa hadi Jumapili huko Hiroshima, ambako ni nyumbani kwa waziri mkuu huyo.

Tayari wakuu mbalimbali wa mataifa wanachama wa G7 wamewasili Hiroshima, mji ulioshambuliwa na bomu la kwanza la atomiki kwa ajili ya mkutano huo unaolenga kujadili pamoja na masuala mengine uwezekano wa kuimarisha vikwazo dhidi ya Urusi na wasiwasi wa kiusalama unaoibuliwa na China. Lakini uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ndio utakaogubika kusanyiko hilo.

Soma Zaidi: G7 yaonya dhidi ya kuubadilisha mfumo wa kimataifa kwa nguvu

Masuala mengine yanatarajiwa kugusia majaribio ya makombora yanayofanywa na Korea Kaskazini na mipango ya nyuklia ya Iran. Viongozi wengine kama waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau na kansela wa Ujerumani pia wamewasili Japan, pamoja na waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak.

Bendera za mataifa wanachama wa G7 wakati wa mkutano wa mataifa hayo nchini Ujerumani, Juni 28, 2022.
Picha: Thomas Lohnes/Getty Images

Biden atasimama mbele ya hadhara hii ya matajiri wa ulimwengu, huku akijaribu kukabiliana na  mgawanyiko aliouacha nyumbani kwake juu ya namna ya kushughulikia ukomo wa deni la taifa hilo. Imemlazimu hata kuahirisha safari yake ya siku nane barani Asia, ili arejee nyumbani mara baada ya mkutano huu wa G7 ili kujaribu kuepusha janga linaloweza kutokea ikiwa Marekani itashindwa kulipa deni lake, hali inayoweza kuutatiza pakubwa uchumi wake na ulimwengu kwa ujumla.

Soma Zaidi:Mawaziri wa G7 wajadili namna ya kuepusha athari iwapo Marekani itashindwa kulipa deni lake la taifa 

Katikati ya kusanyiko hili hata hivyo kunatarajiwa mivutano kutokana na mgawanyiko miongoni mwa wanachama na hasa kuhusu China, hii ikiwa ni kulingana na baadhi ya maafisa waliozungumza na shirika la habari la Reuters, wakati mataifa hayo yatakapokuwa yakiangazia namna ya kulionya taifa hilo dhidi ya kile wanachokiona kama kitisho cha China katika mnyororo wa ugavi wa bidhaa ulimwenguni pamoja na usalama wa kiuchumi bila ya kumtenga kabisa mshirika huyo mwenye nguvu na muhimu kibiashara.

Mataifa ya muungano huo Marekani, Japan, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Canada na Italia wana mafungamano makubwa ya kiuchumi na China, taifa ambalo ni la pili kwa nguvu ya kiuchumi, kitovu cha uzalishaji na hata masoko.