1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Wakuu wa majeshi wa ECOWAS wakutana kuijadili Niger

17 Agosti 2023

Wakuu wa majeshi wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS wanajiandaa kukutana mjini Accra nchini Ghana, kujadili uwezekano wa kuivamia kijeshi Niger, ikiwa juhudi za kidiplomasia zitashindikana.

https://p.dw.com/p/4VGsu
Mkutano wa majeshi wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS
Mkutano wa majeshi wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWASPicha: KOLA SULAIMON/AFP

Mkutano wa wakuu wa majeshi wa nchi wanachama wa ECOWAS unaanza leo na unatarajiwa kumalizika kesho Ijumaa mjini Accra kwenye makao makuu ya jeshi la Ghana.

Wakuu hao wa majeshi wanajadili uwezekano wa kuingiza kikosi cha pamoja nchini Niger kuundowa utawala wa kijeshi uliofanya mapinduzi nchini humo na  kumrudisha rais aliyechaguliwa kidemokrasia Mohammed Bazoum.

Mkutano huu unafuatia maamuzi yaliyofikiwa wiki iliyopita na viongozi wakuu  wa nchi za jumuiya hiyo wa kuandaa hatua za kijeshi kuuingilia kati mgogoro wa Niger  endapo jitihada zote za kidiplomasia zitashindwa. 

Soma pia: Utawala wa kijeshi wa Niger wasema upo tayari kwa mazungumzo 

Watawala wa kijeshi waliofanya mapinduzi Niger wamesema wako tayari kwa mazungumzo lakini bado wanaendelea kumshikilia rais Bazoum na tayari wameshasema watamfungulia mashtaka ya uhaini wa kiwango cha juu, kauli ambayo imetafsiriwa kama ishara inayoonesha watawala hao hawana haja na  juhudi za kidiplomasia katika kuupatia ufumbuzi mgogoro huu.

Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa wote wamezungumzia wasiwasi wao kuhusu hali ya rais Bazoum kutokana na mazingira anayoshikiliwa.

Wachambuzi: ECOWAS inakabiliwa na mgogoro juu ya suala la uhalali

Mkutano wa ECOWAS juu ya kadhia ya Niger
Mkutano wa wakuu wa majeshi wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS mjini AbujaPicha: KOLA SULAIMON/AFP

Wachambuzi kwa upande mwingine wanasema hivi sasa wanachama wa ECOWAS wanakabiliwa na mgogoro kuhusu suala la uhalali wakati taasisi hiyo ikiishiwa mipango na muda wa kurudisha utawala wa kidemokrasia nchini Niger.

Huu ni mkutano wa kwanza kufanywa na wakuu hao wa majeshi tangu viongozi wa ECOWAS walipotowa wiki iliyopita amri ya kupelekwa kikosi cha dharura nchini Niger. Lakini pia haijawa wazi ikiwa kweli kikosi hicho kitaivamia Niger na lini inapangwa kuchukuliwa hatua hiyo.

Kinachozungumzwa ni kwamba kikosi hicho huenda kikajumuisha maelfu ya wanajeshi kutoka Nigeria, Ivory Coast, Senegal na Benin na huenda ikachukuwa wiki kadhaa au hata miezi kukiandaa, kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya migogoro.

Baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika lilikutana Jumatatu wiki hii kutafakari ikiwa linaweza kuunga mkono uingiliaji wa kijeshi lakini mpaka sasa bado halijatowa maamuzi yake hadharani.

ECOWAS kuunda kikosi cha dharura kwa ajili ya Niger

Baraza hilo linaweza kuamuwa kupinga hatua ya kuingiliwa kijeshi Niger ikiwa litahisi uthabiti wa eneo pana katika bara hilo utakabiliwa na kitisho kutokana na hatua hiyo.

Na mtafiti kuhusu masuala ya migogoro Andre Lebovich,anasema  ikiwa litapinga hatua hiyo ya kutumika nguvu za kijeshi basi hapana shaka jumuiya ya ECOWAS itakuwa na nafasi ndogo ya kutowa sababu za msingi za kudai uhalali wa kuingia kijeshi nchini Niger.

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW