ECOWAS yakamilisha mipango ya kuingia kijeshi nchini Niger.
5 Agosti 2023Wakuu wa ulinzi wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, ECOWAS wanakamilisha mipango ya kuingilia kati kijeshi nchini Niger. Wakuu hao wa majeshi ya nchi za ECOWAS wametoa kauli hiyo baada ya mazungumzo na viongozi wa jeshi la Niger kukwama. Viongozi wa jeshi la Niger wamesema wamevunja makubaliano ya kijeshi yaliyofikiwa na Ufaransa. Viongozi hao wa kijeshi wa Niger wamepewa muda hadi hapo kesho kumwachia rais Mohamed Bazoum wanayemshiklilia la sivyo hatua za kijeshi zitachukuliwa dhidi yao na nchi za jumuiya ya ECOWAS. Wajumbe kutoka nchi za jumuiya hiyo waliwasili nchini Niger Alhamisi iliyopita kwa ajili ya mazungumzo ambayo yamekwama baada kushindikana kukutana na kiongozi wa wanajeshi waliotwaa madaraka, Jenerali Abdourahmane Tchiani.