Wakati mwingine utawasikia watu wanaoshiriki ulevi wa pombe wakiulizana, Una kiasi gani cha damu ndani ya pombe yako…? utani huu humaanisha kuwa yule mlevi hunywa pombe nyingi na hii imechukua nafasi ya damu mwilini mwake. Huenda dhana hii ndiyo sasa inawasababisha wataalamu wa ukusanyaji damu kunasibisha hali na watu hao pamoja na makahaba.
Kulingana na wataalamu wa shirika la huduma ya kukukusanya damu, wamegundua kuwa mara nyingi damu ya watu walevi pamoja na makahaba ina maambukizi kama vile virusi vya UKIMWI, kaswende, homa ya damu na kadhalika. Hii ni kutokana na wao kuingiliana kiholela na watu wengine ambao huwambukiza.
Gharama ya kuchunguza ubora wa damu kutoka kwa mtu mmoja ni takriban dola 80 za Kimarekani.
Hii inamaamisha kuwa damu ambayo ina maambukizi hugunduliwa kwa gharama hiyo, jambo ambalo linazidi kutumbukiza nchi katika hasara kubwa. Samuel Wante ni mratibu wa mpango wa ukusanyaji damu.
Lakini mjadala umeibuka kwa mujibu wa hoja kwamba watu wanaoingiliana kimwili na watu wengi ndiyo husababisha damu yao kupata maambukizi.
Ikumbukwe kuwa kuna ndoa za mitara ambapo mume ana wanawake wanne na zaidi.ijapokuwa shirika hilo linadai kuwa watu hao ni waaminifu miongoni mwao, umma umeshindwa kushawishika kuwa makahaba na walevi ndiyo vyanzo vya damu kuambukizwa.
Kwa upande wao, makahaba wanaelezea kuwa baadhi yao hutoa damu mara kwa mara ili kupata taarifa ya hali zao kiafya wakitambua hatari waliomo yakupata maambukizi kutokana na kazi yao.
Mtaalamu wa masuala ya afya Dr. Watiti amefafanua zaidi kuhusu suala hilo.
Kulingana na shirika la afya duniani WHO idadi ya watu wanaotoa damu imeshuka kwa asli mia 17 katika kipindi hiki cha janga la COVID-19.
Nchini Uganda, wanafunzi katika shule na taasisi za elimu ndiyo hutegemewa zaidi kutoa damu. Lakini kwa kuwa shule zimefungwa kwa takriban miaka miwili, imekuwa changamoto kupata kiasi cha kutosheleza mahitaji ya nchi.
Wanawategemea zaidi wanajeshi na polisi kutoa damu siku hizi. Wataalamu wanaelezea kuwa utoaji wa damu wa mara kwa mara ni muhimu kwa afya kwani hupunguza hatari ya damu kuganda, uwezekano wa kuugua saratani sambamba na kupunguza kiwango cha shinikizo la damu. Hali hizi zote ndiyo msingi wa mtu kuishi umri mrefu.