Walia wakiondolewa katika eneo la waasi nchini Syria
25 Machi 2018Wiki tano tangu utawala wa Syria kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya Ghouta , sasa inashikilia zaidi ya asilimia 90 ya eneo hilo ambalo lilikuwa ngome kuu ya upinzani nje kidogo ya mji mkuun Damascus.
Kuusaidia utawala wa Syria kukamata eneo lote, muungano mkono mkubwa wa serikali hiyo Urusi imefanya mazungumzo ya upatanishi na makundi mbali mbali ya waasi kujadili kuhusu kuondoka kutoka katika maeneo matatu yaliyobaki.
Moja kati ya eneo hilo liliondolewa watu chini ya makubaliano hayo katika siku za hivi karibuni na uondoaji wa watu ulianza baadaye siku jana Jumamosi(24.03.2018) kwa sehemu ya pili, inayoshikiliwa na kundi la waasi wenye itikadi kali ya Kiislamu la Faylaq al-Rahman.
Makubaliano hayo yanapagwa kushuhudia kiasi ya waasi 7,000 na raia walichukuliwa kwa mabasi kutoka miji ya Arbin na Zamalka na katika wilaya ya Jobar kwenda katika jimbo linalodhibitiwa na waasi la Idlib kaskazini magharibi mwa Syria.
Baada ya uchelewesho wa masaa kadhaa , kiasi ya raia 980 waliondolewa kutoka Ghouta usiku wa Jumamosi kwa mabasi yapatayo 17 pamoja na magari kadhaa ya kubebea wagonjwa.
Waliwasili katika sehemu ya jimbo la Hama karibu na mpaka na Idlib asubuhi ya Jumapili. Hatua mpya ya kuwaondoa watu inatarajiwa kufanyika leo Jumapili (25.03.2018).
Wabeba vitu vichache
Raia wa Syria waliofadhaika pamoja na wapiganaji wa makundi ya waasi wakivalia mavazi meusi walijikusanya majira ya asubuhi katika mitaa mikuu ya Arbin , mwandishi wa shirika la habari la AFP katika eneo hilo alisema.
Walimebeba mifuko mikubwa na kuburura masanduku yaliyojaa hadi pomoni wakati wakipita katika majengo yaliyoharibiwa. Ilipofika asubuhi , kiasi ya mabasi 20 yaliyokuwa tupu na magari ya kubebea wagonjwa yalikingia katika mji huo, yakiegeshwa katika eneo kubwa la makutano ya barabara.
Wapiganaji na raia walianza kuingia katika mabasi hayo, wakiaga nyumba zao huku machozi yakiwatiririka kabla ya kusafiri kuelekea katika eneo la wapinzani upande wa kaskazini.
Hamza Abbas , mwanaharakati wa upinzani katika mji wa karibu wa Zamalka, aliliambia shirika la habari la AFP anapanga kupanda pia basi na kuondoka.
"Watu wana huzuni sana kwa kuondoka kwenye nyumba zao, ardhi yao , kumbukumbu ya utoto wao na sehemu ambayo waliishi katika nyakati bora kabisa za maisha yao na utoto wao," alisema.
"hawana fedha, hawana nyumba, samani ama hata nguo kuondoka navyo kwasababu ya mashambulizi haya ya mabomu."
Kama sehemu ya makubaliano na kundi la Faylaq al-Rahman na Urusi, wakaazi walipewa fursa ya kubakia mjini Zamalka na Arbin wakati eneo hilo likiangukia katika udhibiti wa serikali.
lakini Abbas alisema hatabakia.
"Niliamua kuondoka Ghouta kwasababu nawezaje kuishi pamoja na mtu ambaye aliuwa familia yangu, watoto watu, marafiki zangu? Na mtu aliyeniharibu, maisha yangu, na hatima yangu?"
Tangu kuanza mashambulizi Februari 18, raia zaidi ya 1,600 wameuwawa na maelfu zaidi wamejeruhiwa, kwa mujibu wa shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Zainab Aziz