Walimwengu waishinikiza Syria izuwie damu isimwagike
30 Mei 2012Damu inaendelea kumwagika nchini Syria-jana tu,wakati mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa na jumuia ya nchi za kiarabu anaendeleza juhudi za kuuokoa mpango wake wa amani,watu wasiopungua 98 wanasemekana wameuliwa-wengi wao ni raia wa kawaida.Na leo pia watu wanne wanasemekana wameuliwa kufuatia mapigano kati ya jeshi na waasi katika kitongoji cha Sitt Zeinab karibu na mji mkuu Damascus.
Kwa upande wa kidiplomasia,uamuzi wa kuwafukuza mabalozi wa Syria, unaonyesha ni wa makubaliano miongoni mwa nchi za umoja wa Ulaya,zikifuatiwa na Marekani,na serikali nyengine za dunia mfano wa Australia,Canada,Uswisi na Japan-na ni jibu la mauwaji ya awali huko Houla ambako watu wasiopungua 108 waliuliwa.
Baada ya mazungumzo pamoja na rais Bashar Al Assad jana,mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa na jumuia ya nchi za kiarabu Kofi Annan ametahadharisha akisema hali inatisha na kuongeza"Wananchi wa Syria hawataki kuwa na mustakbal wao uwe wa umwagaji damu na mgawanyiko.Hata hivyo mauwaji yanaendelea kila kukicha sawa na haki za binaadam zinavyoendelea kuvunjwa."
Mwanadiplomasia hiyo wa kutoka Ghana amewaambia waandishi habari amemhimiza rais Bashar al Assad apitishe hatua madhubuti,kama anavyosema" leo na sio kesho" ili mpango wa amani wa vifungu sita uheshimiwe.
Kofi Annan amesisitiza vikosi vya serikali na makundi yote ya wanamgambo yanayoungwa mkono na serikali yanalazimika kusitisha moja kwa moja harakati zao za kijeshi .
Serikali ya Syria inashinikizwa kutoka kila pembe.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema ataitisha mkutano wa kundi la marafiki wa Syria mwezi July ujao.Amefika hadi ya kusema haondoi uwezekano wa opereshini ya kijeshi,ikiwa itaidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametoa mwito wa kuitishwa kikao chengine cha baraza la usalama kuzungumzia hali namna ilivyo nchini Syria.
Urusi na China zimeshasema hazitoachia uamuzi wowote wa kuingiliwa kijeshi Syria.
Nchi hizi mbili zimekuwa zikilaumiwa kwa kulizuwia baraza la usalama lisipitishe maazimio yaliyopendekezwa na nchi za magharibi kuilaani serikali ya mjini Damascus.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman