Walimwengu wasubiri kuijua hatima ya Brexit
12 Machi 2019Waengereza wanakabiliana na siku ya siku pale bunge lao litakapoyapigia kura makubaliano yaliyofikiwa na waziri mkuu Theresa May, aliyetamka siku moja kabla amefanikiwa kufikia maridhiano pamoja na viongozi wa Umoja wa ulaya mjini Strasbourg kuhusu kifungu kinachohusiana na mpaka kati ya Ireland ya kaskazini na jamhuri ya Ireland au Backstop. Pande hizo mbili, Theresa May na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker wakatangaza "marekebisho yanayodhaminiwa kisheria" ya mkataba wa awali ili kukidhi madai ya waingereza na kwa namna hiyo kufungua njia ya kuungwa mkono bungeni.
Wabunge wahimizwa waunge mkono makubaliano ya Brexit
Wakati umewadia wa kukusanyika na kuunga mkono makubaliano yaliyofanyiwa marekebisho" amesema waziri mkuu Theresa May. Na waziri wake anaeshughulikia masuala ya Brexit, Kwasi Kwarteng akasema ana hakika mwanasheria mkuu Geoffrey Cox ataidhinisha marekebisho hayo:"Nna hakika ataunga mkono mageuzi ya kisheria. Atasema tunaweza kuachana na Backstop tukitaka. Na nna matumaini kutokana na msingi huo DUP, wabunge na wanmachama wa kundi la utafiti kuhusu Ulaya ERG kutoka upande wa wahafidhina nao pia wataunga mkono makubaliano hayo. Sitochoka kusema bunge litabidi lichague leo usiku, ama linaunga mkono makaubaliano ili tusonge mbele au tuendelee na hali isiyojulikana mwisho na vurugu."
Labour wanaendelea kupinga
Hata hivyo chama kikuu cha upinzani Labour kimetangaza kitayapinga makubaliano hayo wakihoji "Theresa May" ameshindwa. Kiongozi wa Labour, Jeremy Corbyn anahoji maridhiano yaliyofikiwa hayana chochote cha maana.
Wenye msimamo mkali ndani ya chama cha kihafidhina cha waziri mkuu Theresa May sawa na wanachama wa DUP, chama kidogo cha jimbo la Ireland ya Kaskazini kinachowakilishwa katika serikali ya muungano mjini London wanasema watadurusu kwa makini marekebisho yaliyofikiwa. Kura imepangwa kupigwa usiku. Akishindwa kwa mara nyengine tena, duru ziada za uchaguzi zitahitajika bungeni wiki hii na penegine kusababisha kucheleweshwa mpango wa kujitoa Brexit au hata kuuakhirisha kwa miezi kadhaa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo