Walinzi wa amani kupungua Darfur
30 Juni 2017Hatua hiyo inayofuata baada ya shinikizo la Marekani, kutokana na hatua yake ya kupunguza Dola Milioni 600, ambazo ilikuwa ikichangia kwenye bajeti ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za kulinda amani. Lilian Mtono na taarifa zaidi.
Baraza hilo kwa kauli moja lilipitisha azimio liloandaliwa na Uingereza ambalo litatumika kupunguza idadi ya wanajeshi na polisi waliopo kwenye operesheni za ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zinazojulikana kama UNAMID, kwa angalau asilimia 30.
UNAMID ina jumla ya wanajeshi 16,000 waliopo Darfur tangu mwaka 2007, walio na jukumu la kulinda raia katika eneo hilo linalokabiliwa na machafuko yaliyosababishwa na mzozo kati ya majeshi ya serikali ya Sudan yaliyopambana sambamba na wanamgambo wa serikali dhidi ya makundi ya waasi.
Mzozo wa Darful kumalizika taratibu
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wanasema kwamba mzozo wa Darfur unamalizika taratibu, na hivyo ujumbe huo wa walinda amani ambao ulikuwa miongoni mwa vikosi vinavyogharimu kiasi kikubwa cha bajeti ya zaidi ya Dola Bilioni 1, unatakiwa kupunguzwa.
Makundi ya haki za binadamu yanaonya kwamba mzozo huo bado una safari ndefu kumalizika, na hatua hiyo ya kuwaondoa walinda amani kutaacha maeneo mengi katika jimbo la Darfur bila ya ulizi wa kimataifa.
"Tunatambua kwamba hali katika eneo la Darfur bado ni tete", amesema naibu balozi wa Uingereza Peter Wilson, na kuongeza kuwa hali ilikuwa imebadilika na mabadiliko hayo yanaakisi hali halisi iliyopo sasa"
Baraza hilo la Umoja wa Mataifa limekubaliana juu ya upunguzwaji wa hatua kwa hatua kwa wanajeshi hao wa UNAMID kutekelezwa kwa awamu mbili ndani ya kipindi cha miezi sita. Hatua ya kwanza itapunguza idadi ya wanajeshi kutoka 13,000 hadi angalau wanajeshi 11,400 katika kipindi cha miezi sita, kabla ya kufikia 8,735 ifikapo mwishoni mwa Juni 2018.
Idadi ya polisi itapungua kutoka 3,150 hadi 2,888 ifikapo Januari na 2500 mwezi Juni mwakani. Wanajeshi watakaosalia watapelekwa katika mkoa wa Jebel Marra, ambako hivi karibuni kumeripotiwa visa vingi vya mapigano.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutterres ataliarifu Baraza la Usalama la Umoja huo baada ya miezi sita kuhusu iwapo hali katika eneo hilo itaruhusu kupunguzwa zaidi wanajeshi.
Baraza hilo pia limeongeza muda wa walinda amani nchini Mali, MINUSMA, na halikuwapunguza wanajeshi hao. Azimio lililoandaliwa na Ufaransa lilipitishwa kwa kauli moja na kuacha wanajeshi 13,3000 na polisi 1,900 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Aidha baraza hilo leo hii limepiga kura ya bajeti mpya ya operesheni za kulinda amani kutoka Dola Bilioni 7.3, kutoka bajeti ya sasa ya Bilioni 7.87.
Katika hatua nyingine, Marekani imesema ina wasiwasi mkubwa kuhusiana na rekodi ya hali ya haki za kibinaadamu nchini Sudan, ambayo ilipaswa kuwa imeimarika kufikia mapema mwezi Julai ili iweze kuondoa vikwazo ilivyoweka dhidi ya nchi hiyo.
Mnamo mwezi wa Januari rais aliyeondoka madarakani, Barack Obama aliipa Sudan siku 180 za kubadilisha rekodi yake na kutatua mzozo wa kisiasa na kijeshi kabla Marekani haijaiondolea vikwazo vya kiuchumi ambavyo viliongezwa mwaka wa mwaka 2006 katika kile kilichoelezwa kuwa ni kuongezeka kwa machafuko katika jimbo la Darfur nchini Sudan.
Mwandishi: Lilian Mtono/rtre/afpe
Mhariri:Yusuf Saumu