Walioambukizwa COVID-19 wafikia zaidi ya laki tatu duniani
22 Machi 2020Janga hili la virusi vya corona limelazimisha mataifa 35 kuwataka wananchi wao wasitoke ovyo nje, na kusababusha kuvurugika kwa hali ya maisha, usafiri na biashara wakati serikali zikijaribu kufunga mipaka na kutoa mamia kwa mabilioni ya dola kama hatua ya dharura ya kuepuka athari ya kuharibika kabisa kwa uchumi kwa kiwango kikubwa.
Zaidi ya maambukizi 300,000 yamethibitishwa duniani kote, ambapo hali inaendele kuwa mbaya nchini Italia ambako idadi ya vifo imepanda hadi zaidi ya watu 4,800, ikiwa ni zaidi ya theluthi ya jumla ya vifo vyote duniani.
Waziri mkuu Gouseppe Conte alitangaza kufungwa kwa viwanda ambavyo havizalishi bidhaa za lazima katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni jana Jumamosi,(21.03.2020).
Taifa hilo la eneo la Mediterania lenye wakaazi wapatao milioni 60 hivi sasa ni kitovu cha ugonjwa huo , ambao kwanza ulijitokeza katikati ya China mwaka jana kabla ya kutoka nje ya mipaka ya nchi hiyo na kusambaa duniani kote.
Italia hivi sasa imeripoti vifo zaidi kuliko China bara na nchi ya tatu Iran kwa pamoja, na ina kiwango cha vifo cha asilimia 8.6 miongoni mwa maambukizi yaliyothibitishwa ya COVID-19, ikiwa ni kiwango cha juu kuliko karibu nchi nyingine.
Nchini Marekani , zaidi ya theluthi moja ya Wamarekani wanajaribu kubadili maisha katika awamu mbali mbali za kufungiwa ndani, ikiwa ni pamoja na miji ya New York , Chicago na Los Angeles. Maeneo mengine ya Marekani yanatarajia kuongeza vizuwizi pia.
"Huu ni wakati wa kujitolea muhanga kwa pamoja, lakini pia ni muda wa kuthamini wapendwa wetu," Rais wa Marekani Donald Trump amesema. "Tutapata ushindi mkubwa."
Dunia yapambana na virusi vya corona
Wakati viongozi wa dunia wameapa kupambana na janga hili, idadi ya vifo na maambukizi vimeendelea kuongezeka , hususan barani Ulaya, kwa hivi sasa ikiwa ndio sehemu hatari ya ugonjwa huo wa virusi vya Corona.
Uhispania imeripoti ongezeko la asimilia 32 katika vifo vipya jana Jumamosi, ambapo waziri mkuu Pedro Sanchez ameonya kuwa taifa hilo linahitaji kujitayarisha kwa kile alichosema "siku zenye matatizo makubwa huko mbeleni".
Vifo nchini Ufaransa vimefikia watu 562 wakati maafisa wa polisi wakisema helikopta na ndege zisizokuwa na rubani zimewekwa kuimarisha juhudi za serikali kuona kwamba watu wanabakia majumbani mwao.
janga hili limevuruga masoko ya fedha ya dunia, na Marekani , ambayo ina uchumi mkubwa duniani , inajitayarisha kuingiza katika uchumi fedha nyingi za kuchochea uchumi ambazo zinaweza kufikia dola trilioni 1. Mamilioni wametakiwa kubakia nyumbani nchini Marekani.
Wakati huo huo kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amekataa msaada wa Marekani leo kupambana na virusi vya corona, akielezea dhana ya njama ambazo hazieleweki kuwa virusi hivyo inawezekana kuwa vimetengenezwa na binadamu kutokea Marekani.
Matamshi hayo ya Ayatollah Ali Khamenei yanakuja wakati Iran inakabiliwa na vikwazo vikali vya Marekani vikizuwia nchi hiyo kuuza mafuta yake ghafi na kuweza kutumia masoko ya kimataifa. Lakini wakati maafisa wa Iran katika siku ya hivi karibuni wamekosoa vikwazo hivyo, Khamenei badala yake ameamua kuleta dhana hiyo ya njama ambayo imekuwa ikitumiwa na maafisa wa China juu ya virusi hivyo vipya katika hatua ya kukwepa lawama kutokana na janga hilo.