Waliohusika katika jaribio la mapinduzi Kongo kushitakiwa
6 Juni 2024Mwendesha mashtaka wa kijeshi mjini Kinshasa amesema kesi hiyo itaendeshwa kwenye gereza la kijeshi lenye ulinzi mkali la Ndolo, katikati mwa jiji kuu la Kongo.
Miongoni mwa washukiwa hao ni pamoja na raia watatu wa Marekanina Muingereza mmoja mwenye asili ya Kongo. Washukiwa hao wanakabiliwa na mashtaka kadhaa yakiwemo ugaidi, mauwaji, kuwa silaha kinyume cha sheria, jaribio la mauwaji na ufadhili wa ugaidi.
Mei 19, jeshi la Kongo lilitangaza kufanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali lililowahusisha raia wa kigeni pamoja na Wakongomani.
Kulingana na msemaji wa jeshi, Jenerali Sylvain Ekenge, karibu watu 50 walikamatwa huku wengine 4 wakiuwawa. Ekenge alisema kwamba njama hiyo iliongozwa na Christian Malanga, ambaye ni mmoja wa waliouwawa.