Waliokufa katika mzozo wa mgodi Afrika Kusini wafika 87
16 Januari 2025Hayo yamesemwa siku ya Alhamisi na polisi wakati wakihitimisha operesheni ya uokoaji ambayo imewaondoa mgodini zaidi ya manusura 240.
Msemaji wa polisi ya kitaifa Athlenda Mathe amesema miili 78 iliondolewa kwenye mgodi huo katika operesheni rasmi iliyoanza Jumatatu, na nyingine ilikuwa imepatikana hapo awali. Bibi Mathe hakutoa maelezo ya jinsi miili hiyo ilivyopatikana.
Mashirika ya kijamii yamesema yalianzisha pia juhudi zao za uokoaji wakati maafisa waliposema mwaka jana kuwa wasingewasaidia wachimbaji hao kwa sababu ni wahalifu. Wachimba migodi hao wanasemekana kufariki kutokana na njaa na upungufu wa maji mwilini.
Maafisa sasa wanaamini kuwa karibu wachimbaji 2,000 walikuwa mgodini humo kinyume cha sheria tangu Agosti mwaka jana. Wengi wao walitoka kwa hiari yao katika miezi michache iliyopita, na manusura wake wamekamatwa.