Waliokufa kwa njaa Kenya wafikia watu 73
25 Aprili 2023Maiti hizo zimefukuliwa kwenye makaburi ya jumuiya yaliyopo msituni. Mkuu wa upelelezi wa kaunti ya Kilifi, mashariki ya Kenya, Charles Kamau amethibitisha idadi hiyo na ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba watu wengine watatu wamekamtwa. Shirika la msalaba mwekundu la nchini Kenya limesema watu 112 hawajulikani walipo. Rais William Ruto amesema kiongozi wa jamii hiyo ya kikristo ni mhalifu mkubwa. Paul Mackenzie alikamatwa takriban wiki mbili zilizopita baada ya fununu juu ya kuwepo kwa makaburi yaliyokuwa na maiti 31 za wafuasi wake. Wafuasi wa kanisa la Good News International walikuwa wanaishi kwa kujitenga kwenye eneo la ekari 800 za msitu wa Shakahola nchini Kenya. Inatuhumiwa kwamba waliagizwa kufunga mpaka kufa ili kuweza kukutana na Yesu. Idara ya upelelezi ya nchini Kenya imesema watu 33 wameshaokolewa hadi sasa.