1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliouawa katika ghasia za Nigeria wafikia 65

Kabogo Grace Patricia27 Julai 2009

Mbali na vifo hivyo, wapiganaji wa Kiislamu wamechoma moto makao makuu ya polisi, kanisa na ofisi ya forodha.

https://p.dw.com/p/IyFj
Polisi wa Nigeria wakifanya doria katika eneo lenye ghasia katika Jimbo la Kano, kaskazini mwa Nigeria, 2007.Picha: AP


Waislamu wenye msimamo mkali katika jimbo la Kano nchini Nigeria mapema leo wamechoma moto makao makuu ya polisi, kanisa moja na ofisi ya forodha katika eneo hilo la Kaskazini mwa nchi hiyo, huku polisi ikitangaza idadi ya watu waliouawa katika ghasia za mwishoni mwa juma kufikia 65.

Akizungumza na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Nigeria, Abuja, Inspekta Jenerali wa Polisi nchini humo, Ogbonna Onovo, amesema kuwa miongoni mwa waliouawa, watano ni askari polisi na 60 ni wapiganaji hao wa Kiislamu wanaojulikana kama Taliban. Inspekta Jenerali Onovo, amesema kuwa vifo hivyo vinawahusisha wale waliouawa katika majimbo ya karibu ya Bauchi na Yobe na kuongeza kuwa mapigano yanaendelea katika jimbo jingine la Borno lililoko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Cameroon.

Inspekta Jenerali Onovo, amesema mapigano hayo yameanza jana Jumapili katika jimbo la Bauchi wakati polisi walipojibizana mashambulizi na wapiganaji hao waliovamia kituo cha polisi. Majibizano hayo ya risasi yalisababisha vifo vya watu 39 na baadaye ghasia hizo zikaelekea katika jimbo la Yobe. Hata hivyo polisi hawajatoa idadi kamili ya watu waliouawa katika kila jimbo. Watu 176 wamekamatwa katika jimbo la Bauchi, kufuatia ghasia hizo zilizosababisha gavana wa jimbo hilo, Isa Yuguda kutangaza amri ya kutotembea usiku kuanzia jana. Yuguda, amesema kuwa amri hiyo itaendelea hadi hapo hali ya usalama na utulivu itakaporejea katika eneo hilo na kuongeza kuwa bila kazi kubwa iliyofanywa na maafisa wa usalama, hali ingekuwa mbaya zaidi.

Kundi hilo la Taliban tawi la Nigeria lilianzishwa mwaka 2004 na kuweka kambi katika kijiji cha Kanamma, Yobe na kuiita kambi hiyo ''Afghanistan'' katika mpaka wa nchi hiyo na Niger, ambako lilivamia vituo vya polisi na kuwaua maafisa wa polisi. Aidha taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa kundi hilo la wapiganaji limevamia kituo kingine cha polisi katika mji wa Wudil nje kidogo ya mji wa Kano.

Msemaji wa polisi wa Kano, Baba Mohammed amesema wafuasi watatu wa kundi hilo wameuawa na wengine 33 kukamatwa. Mohammed amesema askari polisi wawili wamejeruhiwa katika ghasia hizo kwenye mji huo uliopo umbali wa kilometa 30 kutoka Kano. Hali katika eneo hilo ni tete, ingawa askari polisi wanaendelea kufanya doria katika maeneo yote ya jimbo la Kano kuhakikisha kuwa wanarejesha hali ya utulivu.

Eneo la kaskazini mwa Nigeria lina waumini wengi wa Kiislamu, ingawa kuna Wakristo wachache walioko kwenye miji mikubwa, hivyo kuongeza mivutano baina ya dini hizo mbili. Mmoja wa viongozi wa kundi la Taliban tawi la Nigeria, Aminu Tashen-Ilimi, mwaka 2005 aliliambia shirika la habari la AFP katika mahojiano kuwa kundi hilo linataka kuongoza kundi litakaloleta mabadiliko katika jamii iliyokosa uadilifu na isiyo na imani ya kidini.

Tangu mwaka 1999 na kurejea kwa utawala wa kiraia wa serikali kuu ya Nigeria, majimbo 12 ya kaskazini mwa nchi hiyo yalianza kufuata Sheria ya Kiislamu ya Sharia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman