Wamarekani watakiwa kuondoka Yemen
6 Agosti 2013Kwa mujibu wa habari zilizochapishwa katika toleo la mtandao la gazeti la New York Times, wiki iliyopita Marekani iling'amua mazungumzo ya kielektroniki kati ya kiongozi wa mtandao wa al-Qaida Ayman al-Zawahiri, na mkuu wa mtandao huo katika rasi ya Uarabu Nasser al-Wuhayshi, ambamo Zawahiri alimtaka Wuhayshi kufanya mashambulizi haraka, ikiwezekana kabla ya Jumapili iliyopita. Kituo cha televisheni cha Kimarekani CNN, kimesema Zawahiri alimuamuru Wuhayshi kufanya kile alichokiita ''tendo fulani'', agizo ambalo lilichukuliwa na maafisa wa Marekani na wa Yemen kama ishara kwamba mashambulizi yalikuwa yakiandaliwa.
Kitisho hicho kilisababisha kufungwa kwa balozi za Marekani takribani 20 katika nchi za kiarabu. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema 19 kati ya hizo zitaendelea kufunga milango hadi Jumamosi, ikisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa.
Shabaha ya shambulizi badi kitendawili
Christopher Hill kutoka Taasisi ya taaluma ya kimataifa ya Korbel, anaamini Marekani haijui bayana kinakolenga kitisho hicho.
''Hali hii ya kutoa tahadhari kwa ofisi 21 za ubalozi ni ishara tosha kwamba hawajui kwa uhakika wapi mashambulizi hayo yangeelekezwa, na ndio sababu wameamua kujumuisha ofisi nyingi katika kukikabili kitisho hicho.'' Alisema Hill.
Tawi la al-Qaida katika rasi ya uarabu linachukuliwa kuwa lenye kitisho zaidi, baada ya kuvunjwa kwa uongozi mkuu wa mtandao huo nchini Afghanistan na Pakistan mnamo miaka ya hivi karibuni.
Tawi hilo la Yemen limejaribu kufanya mashambulizi kadhaa katika ardhi ya Marekani, na Marekani imejibu kwa kufanya mashambulizi mengi ya kutumia ndege zisizo na rubani, kuwalenga wanamgambo wanaojichimbia katika maeneo yasiyodhibitiwa na serikali ya Yemen.
Washukiwa wauawa
Leo hii ndege isiyokuwa na rubani imeliangamiza gari walilokuwa wakisafiria washukiwa 4 wa ugaidi. Washukiwa hao wote waliouawa wametambuliwa kuwa raia wa Yemen. Haikufamika mara moja iwapo shambulizi hilo linahusiana kwa njia yoyote ile na kitisho kilichosababisha kufungwa kwa balozi.
Taarifa zilizotangazwa na shirika la habari la ABC kwa kumnukuu afisa ambaye hakutaka jina lake litajwe, zimesema kulikuwa na wasiwasi kwamba al-Qaida ilikuwa na mpango wa kuwatumia waripuaji wa kujitoa mhanga, ambao mabomu yameingizwa ndani ya miili yao kwa njia ya upasuaji, ili kuweza kuepa ukaguzi.
Ofisi za ubalozi wa Marekani ambazo zilifungwa kutokana na kitisho hicho ni zile zilizo katika nchi za Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Saudi Arabia na Qatar. Nyingine ni Kuwait, Bahrain, Oman, Yemen na Libya. Hali kadhalika Balozi za Marekani huko Madagascar, Burundi, Rwanda, Djibouti, Sudan na Mauritius ziliathiriwa na kitisho hicho.
Balozi katika nchi sita, Afghanistan, Algeria, Bangladesh, Mauritania, Iraq na Israel zimefunguliwa. Ulinzi mkali zaidi umewekwa katika Ubalozi wa Marekani nchini Yemen, na Marekani imewataka raia wake waondoke nchini humo mara moja.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman