1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamisri waapa kurejea Tahrir

19 Juni 2012

Mchakato wa kuelekea demokrasia nchini Misri ambao tayari umekumbwa na wahaka ulitumbukizwa katika ghasia siku ya Alhamis baada ya mahakama ya katiba kubatilisha bunge katika kile kilichoitwa mapinduzi ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/15Fja
Mchakato wa kuelekea demokrasia nchini Misri ambao tayari umekumbwa na wahaka ulitumbukizwa katika ghasia hapo jana na hukumu hii ya mahakama ya katiba, huku wanaharakati wa kiislam ambao ndiyo wanadhibiti Bunge la nchi hiyo, na waliyonufaika zaidi na kuondolewa kwa Hosni Mubarak wakiita hukumu hiyo mapinduzi laini.
Wandamanaji na maafisa usalama wakiwa nje ya mahakama ya katiba mjini Cairo.Picha: picture-alliance/dpa

Vyama vya siasa na wanaharakati nchini humo wameitisha mandamano makubwa siku ya Ijumaa kupinga hukumu hiyo ambayo kimsingi imerejesha majukumu ya kutunga sheria kwa Baraza la kijeshi. Katika hukumu hiyo mahakama pia ilibatilisha sheria iliyowapiga marufuku maafisa wa juu katika utawala wa Hosni Mubarak kushiriki siasa, na hivyo kumsafishia njia Ahmed Shafique, Waziri Mkuu wa mwisho wa Hosni Mubarak.

Vuguvugu la vijana la Aprili 6 na lile la Kisoshalisti walitangaza kufanya mandamano yaliyopewa jina la 'Pamoja dhidi ya Mapinduzi laini ya Kijeshi' yakilenga kupinga uamuzi huu wa mahakama hiyo ya juu. Mamia ya wanadamanaji walishaanza kukusanyika katika viwanja vya Tahrir mjini Cairo. ambavyo vilikuwa kituo kikuu cha mapinduzi yaliyomg'oa Hosni Mubarak.

Ahmed Shafik.
Ahmed Shafik.Picha: picture-alliance/dpa

"Tulifanya mapinduzi na hakuna mapinduzi yoyote duniani yanayorejesha utawala wa kibabe. Baraza la kijeshi linataka kurejesha utawala wa zamani, na wanataka turudi kuwa watumwa. hatutorudi kuwa watumwa, tutaendelea kupambana, na kupambana dhidi ya Ahmed Sahfique, na tutaendelea. Mungu akipenda," alisema Mohammed Hussein.

Uchaguzi kuendelea kama ilivyopangwa
Wamisri wanatarajiwa kupiga kura siku ya Jumamosi na Jumapili katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais ambapo Ahmed Shafique anapambana na mgombea kutoka chama cha Udugu wa Kiislam, Mohammed Mursi. Shafique amabye ni Jenerali wa zamani wa jeshi alikaribisha hukumu hiyo ya mahakama na kuongeza kuwa ulikuwa wa kihistoria.

Wandamanaji wakiwa katika viwanja vya Tahrir kupinga utawala wa kijeshi.
Wandamanaji wakiwa katika viwanja vya Tahrir kupinga utawala wa kijeshi.Picha: dapd

Mohammed Mursi ambaye alisema ataendelea kuwemo katika kinyanganyiro hicho cha urais, aliielezea hukumu hiyo pamoja na amri za hivi karibuni za serikali kwa jeshi na maafisa wa Intelijensia kukamata raia, kama hujuma dhidi ya matakwa ya watu wa Misri.

Kundi la vyama sita vya siasa lilitoa taarifa likisema kuwa Baraza Kuu la kijeshi (SCAF) limedhamiria kurudihsa utawala wa zamani na kwamba uchaguzi unaofanyika mwishoni mwa wiki hii ni geresha tu. Vyama hivyo, kikiwemo cha Uhuru na haki vimemtaka Mgombea wa Udugu wa Kiislam Mohammed Mursi kujiondoa katika kinyanganyiro hicho.

Kundi hilo limewataka pia wabunge wote kujiunga na wanamapinduzi dhidi ya utawala wa kibabe wa majenerali wa kijeshi. Hukumu hii imezidi kuleta mchanganyiko kwa vile hata mamlaka ya rais atakayechaguliwa yalitakiwa kubainishwa na Baraza la katiba ambalo liliteuliwa na Bunge wiki iliyopita.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\RTRE\DPAE
Mhariri: Saum Yusuf.