Wamorocco 3 wafungwa kwa ubakaji Cologne
24 Februari 2016Katika hukumu hizo za kwanza tangu kutokea kwa mkasa huo, mahakama ya mji wa magharibi mwa Ujerumani, Cologne, ilitoa hukumu ya kifungo cha nje cha miezi sita na faini ya euro 100, kwa kijana wa kwanza Mmoroco aliye na miaka 23 aliyekubali kumuibia mwanamke mmoja simu ya mkononi.
Katika kesi nyengine mbili ambazo pia zinahusiana na wizi na sio unyanyasaji wa kimapenzi, mwanamume mmoja raia wa Tunisia aliye na miaka 22 na Mmoroco mwengine wa miaka 18 walidaiwa kuiba kamera katika mfarakano uliyotokea nje ya mji wa Cologne katika kituo cha treni na uwanja wa kanisa kuu la kikatoliki mjini humo.
Majina ya washukiwa hao hayajatolewa ikiwa ni kwa sababu ya sheria ya Ujerumani inayohusiana na uwekaji siri masuala nyeti.
Vurugu hizo ziliongeza wasiwasi nchini Ujerumani, ambayo imewachukua waomba hifadhi zaidi ya milioni moja mwaka wa 2015, wengi wao kutoka Syria, Afghanistan na Iraq, huku kansela wa Ujerumani Angela Merkel akilaumiwa kwa uamuzi wake wa kuwakaribisha wakibizi wanaokimbia mapigano nchini mwao.
Polisi yakosolewa
Polisi mjini Cologne imekosolewa vikali kwa kushindwa kuzuwia visa vya halifu uliyotokea, na kisha kukataa kwa siku kadhaa. Aliyekuwa mkuu wa polisi mjini humo Wolfgang Albers alisimamishwa kazi kwa muda katika harakati za kurejesha imani ya wananchi ndani ya vikosi vya usalama. Polisi imepokea malalamiko mengi juu ya kisa hicho.
Hata hivyo polisi imewatambua washukiwa 75 wa uhalifu huo, na kuwakamata watu 13 wanaoshukiwa kuhusika katika vitendo vya wizi lakini kesi moja tu ndio inayohusika na udhalilishaji wa kingono.
Akizungumza na Shirika la utangazaji la Uingereza BBC Mkuu wa Polisi Juergen Mathies amesema washukiwa wengi wa visa vya unyanyasaji wa kimapenzi huenda wasigundulike kutokana na kile kilichomo ndani ya video kutoonekana vizuri na kukosekana mashahidi waliyoshuhudia visa hivyo. Mathies amesema ni vigumu kuwatambua wahalifu hao.
Aidha kutokana na visa hivyo vilivyotokea mjini Cologne serikali ya Ujerumani imelifanya kuwa jambo rahisi hivi sasa kuwarejesha katika nchi zao wanakotoka wageni wanaopatikana na makosa ya uhalifu.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman