Wanafunzi 3 kati ya 6 waliotekwa nyara Uganda watoroka
21 Juni 2023Familia za wanafunzi watatu ambao wameweza kuwaponyoka watekaji wao zina furaha kubwa ila wale ambao watoto wao wangali hawajulikani waliko wapo katika majonzi. Msemaji wa jeshi la Uganda brigedia Felix Kulayigye ameiambia DW kwamba wanafanya kila juhudi kuwafuatilia mateka hao .
Wanafunzi manusura wanaendelea kupata matibabu
Wakati huohuo, wanafunzi manusura wa kisa hicho wanaendelea kupata matibabu katika hospitali kuu ya wilaya ya Kasese huku wakisimulia jinsi walivyonusurika.
Hapo awali palikuwa na wazo kuwa wavamizi hao walikuwa genge lililokodishwa kufanya mauaji hao kutokana na mvutano wa umiliki wa shule hiyo. Lakini msemaji wa jeshi amefahamisha kuwa sasa wamethibitisha wavamizi hao ni wa kundi la waasi wa ADF ambao huvamia na kuwauwa raia katika nchi ya Congo.
Vikosi zaidi vyatumwa Kasese
Msemaji huyo ameongeza kuwa wametuma vikosi zaidi vya wanajeshi eneo la Kasese kuwahakikishia wananchi usalama dhidi ya visa vya uvamizi. Hii leo, waziri wa ulinzi anatarajiwa kuwasilisha taarifa rasmi katika bunge la Uganda kuhusu kisa hicho. Kwingineko, mwanamume mmoja aliyesambaza habari kwenye jukwaa la kijamii la Tik Tok akidai kuwa alikuwa miongoni mwa kundi la ADF lililofanya shambulizi hilo la kikatili lililowauwa watu 42 amekamatwa na polisi.