1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati wapinga ripoti ya tume ya serikali ya mto Mara

Florence Majani23 Machi 2022

Wadau wa haki za binadamu na wadau wa mazingira nchini Tanzania, wametoa tamko la pamoja kuipinga ripoti iliyotolewa na kamati iliyoundwa na serikali kwa ajili ya  kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji ya mto Mara.

https://p.dw.com/p/48vy3
DW Sendung Eco Africa Mara River in Tansania
Picha: DW

Awali, Mwenyekiti wa kamati hiyo iliyoundwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Seleman Jafo, Profesa Samuel Manyele alisema kuwa chanzo cha uchafuzi wa maji ya mto huo ni uwepo wa kinyesi cha ng'ombe zaidi ya tani 1.8 milioni pamoja na mkojo wa ng'ombe lita 1.5 bilioni uchafu uliotokana na kuwepo kwa ng'ombe zaidi ya laki 3 waliopo mkoani Mara.

Hata hivyo, akizungumza katika mkutano na wanahabari leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) Wakili Ana Henga, aliikosoa ripoti ya Profesa Manyele na kusema imejaa upotoshaji na ni kejeli kwa akili za Watanzania kwani kamati hiyo iliundwa kwa ajili ya kuwaficha wachafuzi wa mazingira.

Henga alisema taarifa za kukinzana pia zinaifanya ripoti hiyo kuibua maswali zaidi baada ya kuwepo ripoti ya bonde la maji la Ziwa Victoria, ambapo ripoti ya bonde la maji inaonyesha uchafuzi huo umetokana na mafuta ya grisi wakati ile ya Prof Manyele ni kutokana na kinyesi cha mifugo.

 Ripoti yenye upotoshaji ?

Ripoti ya tume ya uchunguzi wa mto Mara yazua maoni mseto
Ripoti ya tume ya uchunguzi wa mto Mara yazua maoni msetoPicha: DW/L. Osborne

Kamati hiyo ilishindwa kueleza picha za samaki waliokufa zimetoka wapi na wakasema wanashangazwa na ripoti hiyo kueleza ni kwa namna gani kinyesi cha ng'ombe kimesababisha uchafuzi huo hadi kusababisha ng'ombe hao hao kufa.

LHRC na Chama cha Wanasheria Wanaharakati wa Mazingira (LEAT ) wametoa maazimio 12 ya pamoja kwa serikali na baadhi ni haya yaliyosomwa na Mkurugenzi wa LEAT, Dk Rugemeleza Nshala.

Kabla ya kutoa tamko hili, LHRC  na (LEAT) walifanya utafiti mdogo na kutembelea vijiji  vinavyotegemea maji ya Mto Mara, hasa vijiji vya Kirumi na Busari na kubaini vifo vya mifugo zaidi ya 800  kati ya mwaka 2018 hadi 2022 kwa kunywa maji yanayodhaniwa kuwa na sumu.

 Kadhalika katika kipindi kati ya Machi 1 hadi Machi 15ngombewalifariki kwa kunywa maji hayo. Kati ya mwaka 2020 hadi 2021, NUSU YA wakazi wa vijiji hivyo walipata ugonjwa wa ngozi, uliofahamika kwa jina la ‘Kwangua Vocha' uliowafanya kujikuna na ngozi. Pia baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo walifariki wakidaiwa kunywa maji hayo na baadaye kutapika damu na kuharisha.