1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi kuongoza kipindi cha mpito cha miaka mitatu Mali

Saleh Mwanamilongo
24 Agosti 2020

Wanajeshi nchini Mali wanataka kuweko na kipindi cha mpito cha miaka mitatu kitakachoongozwa na mwanajeshi,wameridhia pia kumuachia huru rais Keita na waziri mkuu wake.

https://p.dw.com/p/3hPQl
Mali Bamako Verhandlungen zwischen ECOWAS und Militärführern | Goodluck Jonathan
Picha: Reuters/M. Kalapo

Wanajeshi waliochukuwa madaraka nchini Mali wanataka kuweko na kipindi cha mpito cha miaka mitatu kitakachoongozwa na mwanajeshi. Kufuatia mazungumzo na ujumbe wa Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika ya magharibi,ECOWAS,wanajeshi hao wanaridhia kuachiwa huru kwa rais Ibrahim Boubacar Keita na waziri mkuu wake.

Wanajeshi hao waliochukuwa madaraka siku ya Jumanne wanashikilia kwamba serikali mpya itakayoundwa itajumuisha maafisa wengi wa jeshi. Kuhusu hatma ya rais Ibrahim Boubacar Keita na waziri mkuu wake Boubou Cissé wanaoshikiliwa hadi sasa kwenye kambi ya kijeshi ya Kati, nje kidogo ya mji mkuu Bamako, wanajeshi hao wanasema wako tayari kuwaachia huru.

Baada ya kipindi cha masaa kumi ya majadiliano Jumapili, kiongozi wa ujumbe wa jumuiya ya ECOWAS, Goodluck Jonathan, anasema kwamba kuna matumaini ya kuweko na muafaka kuhusu vipengee kadhaa vinavyojadiliwa.

''Sote tunataka Mali kupiga hatua kwenda mbele, pande zote ikiwemo ujumbe wa ECOWAS na viongozi wapya wa nchi. Tumekubaliana kuhusu masuala kadhaa lakini bado kuna baadhi ya mambo ambayo tunaendelea kuyajadili. Tutawapa taarifa zaidi wakati kila kitu kitakapokamilika.''

Makubaliano yatarajiwa jumatatu

Mali Bamako Verhandlungen zwischen ECOWAS und Militärführern | Assimi Goita
Picha: Reuters/M. Kalapo

Kwa upande wake kanali Ismael Wague ambaye ni msemaji wa jeshi lililo uongozini kwa sasa ambalo kwa sasa linajiita Kamati ya Kitaifa ya Ukombozi wa Watu, amesema pia kwamba mazungumzo yanaendelea vyema.

''Tunakubaliana kuhusu baadhi ya mambo na mazungumzo yataendelea na tunategemea kutakuweko na makubaliano.''

Duru ya tatu ya mazungumzo baina ya wanajeshi na ujumbe wa jumuiya ya ECOWAS inapangwa kufanyika baadaye leo. Mkuu wa kamisheni ya ECOWAS Jean-Claude Kassi Brou amesema mazungumzo ya Jumamosi na Jumapili yalifanyika katika mazingira ya uwazi na walihisi haja ya kuendelea mbele. Kassi Brou ameongeza kwamba wanatazamia kukamilisha kila kitu kufikia leo Jumatatu.

Kikao kipya cha marais wa Jumuiya ya ECOWAS

Marais wa nchi 15 za jumuiya hiyo ya ECOWAS wanatarajiwa kukutana Jumatano ili kuamua kuhusu vikwazo walivyoiwekea Mali.

Jumuiya ya ECOWAS ilichukua msimamo mkali dhidi ya wanajeshi walioiangusha serikali ya rais Keita, kwa kuifunga mipaka ya nchi hiyo na kuzuia mtiririko wa fedha kuingia Mali.

Soma zaidi: Ujumbe wa ECOWAS waelekea Mali kuzungumza na wanajeshi

Mapinduzi hayo yaliyomuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita yalilaaniwa na jumuiya ya kimataifa, lakini yalishangiliwa katika nchi hiyo inayokabiliwa na uasi wa kijihadi pamoja na mtafaruku wa kisiasa.