1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Urusi wawasili Syria

25 Oktoba 2019

Wizara ya ulinzi ya Urusi inasema karibu wanajeshi mia tatu wa nchi hiyo wamewasili Syria Ijumaa chini ya makubaliano kati ya Uturuki na Urusi yaliyosimamisha operesheni za kijeshi kaskazini mashariki mwa Syria.

https://p.dw.com/p/3Rv69
Syrien Amuda russische Truppen patrouillieren im Norden
Picha: AFP/D. Souleiman

Makubaliano hayo yaliyofikiwa Jumanne na marais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Vladimir Putin wa Urusi yanahitaji jeshi la polisi na Urusi na walinzi wa mpakani wa Syria wawaondoe wanamgambo wote wa Kikurdi wa YPG katika eneo lililo kilomita thelathini kutoka mpaka wa Uturuki kufikia Jumanne ijayo.

Hapo Alhamis wanamgambo wa YPG waliituhumu Uturuki kwa kufanya mashambulizi ya ardhini yaliyovilenga vijiji vitatu kaskazini mashariki mwa Syria licha ya makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano, jambo lililosababisha kukimbia kwa maelfu ya raia.

Trump amekosolewa na wengi kwa alichoandika kwenye Twitter

Wakati ambapo viongozi wa Urusi na Uturuki wakiwa wanaungana kuhakikisha kuna usalama kaskazini mashariki mwa Syria kufuatia hatua ya Marekani kuviondoa vikosi vyake, Rais wa Marekani Donald Trump yeye fahamu zake ziko kwenye visima vya mafuta kwengineko katika nchi hiyo iliyozongwa na vita.

Erdogan und Putin in Sochi
Rais Erdogan wa Uturuki (kushoto) na Rais Putin wa Urusi (kulia)Picha: Reuters/S. Chirikov

Hapo Alhamis Trump alikosolewa na wengi kufuatia ujumbe aliouandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter akisema kwamba alizungumza na mkuu wa jeshi la Wakurdi nchini Syria Mazloum Abdi na kuonelea kwamba labda sasa ni wakati ambapo Wakurdi wanastahili kuelekea katika eneo lenye mafuta nchini humo.

Rais Erdogan wa Uturuki ni mmoja wa wale waliomkosoa Trump kwa hatua hiyo.

"Kwa upande mmoja sisi tunajadiliana kuhusu kupambana na magaidi na kwa upande mwingine nyinyi munaifungua milango kwa magaidi hao, munakuja kwenye meza ya mazungumzo nao na hata munatumiana barua. Tayari tumezungumza na Trump moja kwa moja kuhusiana na jambo hili na tumemwambia kwamba tumevunjwa moyo na hatua hii," alisema Erdogan.

Uturuki inawalazimisha wakimbizi kurudi Syria

Lakini licha ya Trump kushinikiza kuondoka kwa karibu vikosi vyote vya Marekani nchini Syria, amevitaja zaidi ya mara moja visima vya mafuta vya nchini humo kama ardhi yenye umuhimu ambayo ananuia kuilinda.

Syrien Amuda russische Truppen patrouillieren im Norden
Vikosi vya wanajeshi wa Uturuki vikipiga doria Syria kaskaziniPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Ahmad

Huku hayo yakiarifiwa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu lililo na makao yake mjini London Amnesty International limesema Uturuki inawapeleka kwa lazima wakimbizi wa Syria katika eneo lililo karibu na mpakani ambako wanalenga kuweka eneo salama licha ya kuwa machafuko bado yanaendelea katika eneo hilo.

Amnesty linasema wakimbizi waliozungumza nao wamelalamikia kutishwa au kulazimishwa na polisi wa Uturuki kutia saini nyaraka zinazosema wanarudi Syria kwa hiari.

Kwa sasa Uturuki inawapa hifadhi wakimbizi milioni 3.6 kutoka Syria.