Wanajeshi wa Uturuki wapatiwa hifadhi Ujerumani
9 Mei 2017Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani haikuweza mara moja kupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Sueddeutsche Zeitung pamoja na vituo vya televisheni vya taifa vya WDR na NDR, maafisa wamethibitisha kwamba Ujerumani imetoa ishara zinazoelekeza kwamba maombi yao hifadhi yatakubaliwa kwa raia hao wa Uturuki.
Wanajeshi hao pamoja na familia zao ambao wanahifadhiwa katika maeneo yaliyotayarishwa na NATO nchini Ujerumani, wamepatiwa hifadhi katika uamuzi wa awali wa kuomba hifadhi. Wanajeshi hao wa Uturuki waliomba hifadhi nchini Ujerumani baada ya kukabiliwa na mashitaka kufuatia jaribio la mapinduzi lililoshindwa Julai 15, mwaka 2016.
Vyombo vya habari vya Ujerumani vimesema kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani jumla ya maombi 414 yamewasilishwa na wanajeshi hao wa Uturuki , wanadiplomasia, majaji na maafisa wengine wa serikali wanaoishi nchini Ujerumani. Idadi hiyo inaripotiwa kuwajumuisha pia wanafamilia wa waombaji hifadhi.
Wizara ya mambo ya ndani pia imeeleza kwamba jumla ya watu 262 miongoni mwa wanaoomba hifadhi ni maafisa wa Uturuki wenye pasi za kusafiria za kidiplomasia, lakini haikusema ni maombi kiasi gani yamekuja moja kwa moja kutoka kwa wanajeshi wa Uturuki walioko katika vituo vya NATO.
Hakuna ishara juu ya kiasi gani cha maombi yamekubaliwa , ama maelezo ya moja kwa moja kutoka kwa maafisa wa serikali ambao wanahusika moja kwa moja na kushughulikia maombi hayo , ofisi ya shirikisho inayohusika na wahamiaji na wakimbizi (Bamf).
Maafisa wa Uturuki walianzisha msako mkubwa baada ya jaribio la mapinduzi, ambalo lilishuhudia maelfu ya wale wanaodaiwa kuwa wanajeshi wanaomunga mkono imamu anayeishi uhamishoni nchini Marekani Fethullah Gülen walikamatwa ama kufutwa kazi nchini Uturuki, ambao serikali inawaona kuwa ni washirika wa njama za jaribio hilo lililoshindwa la mapinduzi.
Kwa mujibu wa ripoti hizo za vyombo vya habari , maafisa wa Bamf walisubiri matokeo ya kura ya maoni yenye utata kuhusiana na mabadiliko ya katiba ya Uturuki kabla ya kuchukua uamuzi kuhusu maombi hayo ya wanaotaka hifadhi ya kisiasa.
Maafisa hao lakini wanakana kwamba kulikuwa na uhusiano wa aina yoyote kuhusiana na suala la mabadiliko ya katiba. Matokeo ya kura hiyo ya maoni imempa ushindi mwembamba rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuwa na madaraka mapya chini ya mfumo wa uongozi wa rais. Wakosoaji wanahofu kwamba Erdogan huenda akatumia vibaya mfumo huo mpya kukandamiza zaidi sauti za upinzani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / English page / afpe
Mhariri : Iddi Ssessanga