Wanajeshi wakamata watawa nchini Myanmar.
27 Septemba 2007Kiasi cha watu wa kawaida 10,000 walikusanyika katika eneo karibu na eneo la Sule Pagoda , eneo ambalo lilikuwa kwa muda wa siku 10 likifanyika maandamano , ambapo walikuwa wakipiga kelele na kuwakejeli wanajeshi wa serikali huku wakipiga makofi kuonyesha kutoridhishwa kwao na majeshi hayo kuzingira hekalu la ibada za dini ya Kibudha.
Japokuwa vizuizi vimeondolewa katika barabara hiyo ya Pagoda leo Alhamis asubuhi , kulikuwa na polisi wenye silaha na wanajeshi waliojipanga kandokando ya barabara hiyo , na ambao wamewekwa mahsusi katika hekalu hilo la Pagoda , tayari kukabiliana na ghasia.
Wakati huo huo , kiasi cha wanakijiji 1,000 kusini mwa mji wa Okkalapa nje kidogo ya mji wa Rangoon wamelishambulia lori la wanajeshi , wakiwarushia mawe wanajeshi hao hadi pale walipofyatua mabomu ya kutoa machozi katika kundi hilo na kufanikiwa kuondoa kwa haraka gari lao.
Wanakijiji hao wanaripotiwa kuwa wamechukizwa kuwa wanajeshi walivamia nyumba ya watawa wa Ngwe Kyar Yan asubuhi ya leo , na kuwakamata watawa na kumwacha mkuu wa watawa hao akiwa amepigwa sana na kujeruhiwa.
Wako watu ambao wako tayari kushambulia na wako ambao wako tayari kufa, amesema mwanadiplomasia mmoja kutoka mataifa ya magharibi akizungumzia hali inayokaribia kuonekana ya mapambano mjini Rangoon.
Ilisikika asubuhi ya leo milio ya risasi karibu na kituo kikuu cha treni mjini Rangoon.
Wengi wa watawa hawakujitokeza leo Alhamis katika maandamano , huku kukiwa na ripoti kuwa maafisa wamevamia nyumba kadha za watawa asubuhi ya leo , na kuwakamata kiasi cha watawa 100. Maafisa wa usalama walivamia nyumba ya watawa ya Moe Kaung katika mji wa Yankin na Ngwe Kyar Yan kusini mwa mji wa Okkalapa na kuwachukua watawa katika malori, ambayo yamefukikwa maturubai.
Watu walioshuhudia wamesema kuwa watawa hao walipigwa na kuburuzwa wakati wakitolewa nje ya nyumba zao huku wakipiga mayowe.
Michirizi ya damu ilionekana wazi katika nyumba hizo za watawa. Utawala wa kijeshi uliamua kupambana dhidi ya maandamano hayo yanayoongozwa na watawa ambayo yalianza kwa kiwango kidogo hapo Septemba 18 na kushika kasi Jumatatu iliyopita kukiwa na waandamanaji wanaokadiriwa kufikia 100,000.
Jana Jumatano polisi wa kuzuwia ghasia na wanajeshi waliwapiga watawa pamoja na wafuasi wao watu wa kawaida kwa virungu na mabomu ya moshi wa kutoa machozi katika eneo la Shwedagon Pagoda na kufyatua risasi hewani za tahadhari dhidi ya kundi la waandamanaji katika eneo la Sule Pagoda. Gazeti linalochapishwa na serikali la New Light limedai kuwa mapambano hayo yalizushwa na waandamanaji waliowatupia mawe maafisa wa usalama.