1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wanyang'anywa silaha CAR

Mjahida16 Februari 2014

Wanajeshi wa kulinda amani wa Kimataifa walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati wameingia nyumba hadi nyumba Bangui, kuwanyang'anya silaha wanamgambo wanaoshutumiwa kutekeleza visa vya uhalifu dhidi ya Waislamu waliowachache.

https://p.dw.com/p/1B9u2
Baadhi ya wanajeshi wa kulinda amani
Baadhi ya wanajeshi wa kulinda amaniPicha: Reuters/Siegfried Modola

Oparesheni hiyo ya kipekee ilifanywa na wanajeshi wa kulinda amani takriban 250 pamoja na polisi katika eneo jirani la Boy Rabe mjini Bangui, eneo linalokaliwa na wanamgambo wa Kikristo.

Mashambulizi kutoka kwa Wanamgambo hao yamesababisha Waislamu kuukimbia mji huo katika wiki za hivi karibuni.

Kulingana na Mwanasheria mkuu wa serikali Ghislain Gresenguet, mabomu pamoja na silaha nyingine zilipatikana huku watu kadhaa wakitiwa nguvuni.

Kwa upande wake mmoja wa wanajeshi wa Umoja wa Afrika katika kikosi cha MISCA aliliambia shirika la habari la AFP watu wote waliopatikana na silaha wametambuliwa na watafikishwa polisi.

Manusura wa mashambulizi Jamhuri ya Afrika ya Kati
Manusura wa mashambulizi Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: picture alliance/Amnesty International

Wanamgambo wa "anti-balaka" walijikusanya katika nchi hiyo ilio na idadi kubwa ya wakristo kujibu mashambulizi ya mauaji yanayodaiwa kufanywa na waasi wa kiislamu wa Seleka baada ya kuuangusha utawala wa rais Francois Bozize katika mapinduzi ya Machi mwaka 2013.

Katika miezi ya hivi karibuni, kundi la wanajeshi wa Kimataifa waliopelekwa katika taifa hilo ambalo ni koloni la zamani la Ufaransa, wamefanikiwa kusimamisha mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na waasi wa Seleka na wanamgambo wa Kikristo hali iliosababisha hofu miongoni mwa Waislamu.

Catherine Samba Panza, atangaza vita dhidi ya kundi la anti balaka.

Rais wa mpito katika Jamhuri hiyo ya Afrika ya Kati Catherine Samba Panza, ambaye ni Mkristo, wiki iliopita alitangaza vita dhidi ya kundi la anti balaka. Mashambulizi ya kundi hilo yamesababisha kutolewa onyo la kutokea ghasia za kidini.

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema operesheni ya jeshi la nchi hiyo katika Jamhuri ya Afrika ya kati zitakuwepo kwa muda mrefu kuliko ilivyopangwa hapo awali. Siku ya Ijumaa Ufaransa ilisema itatuma wanajeshi wake wengine 400 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba Panza
Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba PanzaPicha: Eric Feferberg/AFP/Getty Images

Takriban watu milioni moja wamepoteza makaazi yao kutokana na mapigano kati ya makundi ya waasi wa Kiislamu wa Seleka na wanamgambo wa Kikristo. Watu takriban 2000 wameuwawa katika ghasia hizo za kidini tangu mwezi wa Desemba mwaka uliopita.

Ufaransa na Umoja wa Ulaya umeahidi kuongeza idadi ya wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Kiafrika wakati kukiwa na visa vya kuogofya katika ghasia za nchi hiyo. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel jana alisema Berlin ilihitaji kupiga jeki ushirikiano wake wa kijeshi na Ufaransa hasaa barani Afrika.

"Mahusiano yetu ya karibu yanawezekana", Alisena Kansela wa Ujerumani huku akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni wa kuungana pamoja katika mataifa ya Mali, ama Jamhuri ya Afrika ya kati.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo